MTANDAO wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Dodoma (NGONEDO) umetambulisha mradi wake wa mapitio ya hatua zilizofi kiwa na wadau pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma juu ya uboreshaji wa huduma za maji.
Hiyo ni kutokana na mradi wa kujengea uwezo jamii na asasi za kiraia katika kufuatilia raslimali za umma (PETS) katika miradi ya maji wilayani humo. Akizungumza wakati wa mkutano wa kutambulisha mradi huo mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Bahi, Dk Fatma Mganga, Mratibu wa Ngonedo, Edward Mbogo alisema mradi huo unalenga kufanya mapitio na kufuatilia matokeo ya kufuatilia matokeo ya utekelezaji wa miradi ya maji uliofanyika katika kata nne ili kuona mafanikio.
Pia ufanisi na changamoto zake na hatimaye kuwa na rejeo bora namna bora ya kutekeleza miradi ya kijamii kwa lengo la kuonesha urejesho chanya kwa jamii. Pia alisema mradi huo unalenga kupata rejea na kujifunza kwa maslahi ya pande zote na ni namna gani bora zaidi ya kuitekeleza miradi hiyo na jamii iweze kutoa tija bora na chanya pasipo kuathiri umuhimu wake kwa jamii.
Alisema malengo mengine mahususi ni kujua hatua gani zimechukuliwa na wananchi pamoja na Halmashauri ya Bahi katika kuboresha huduma za maji kwa mtazamo wa sera na sheria ya maji.
Mbogo alisema mradi huo utatekelezwa katika Wilaya ya Bahi katika kata nne, Bahi, Mpamantwa, Mundemu na Msisi na vijiji vinne vya Bahi, Mkakatika, Mchito na Nguji.
Alisema mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi sita kuanzia Julai 2020. Walengwa wa mradi ni asasi za kiraia, jamii, wajumbe wa kamati za PETS kutoka kata nne na vijiji vinne.