Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi mpya wa 'Mwendokasi' kupoza makali ya usafiri Dar

Mkuranga Mwendokasi Mradi mpya wa 'Mwendokasi' kupoza makali ya usafiri Dar

Wed, 23 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ujenzi wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) awamu ya tano wenye thamani ya Euro 178 milioni (Sh427 bilioni), unatarajiwa kuanza Desemba mwaka huu na kukamilika ifikapo mwaka 2025.

Ujenzi wa awamu ya tano wenye urefu wa kilomita 26, utaanzia katika makutano ya daraja la juu la Kijazi Ubungo kupitia Barabara ya Mandela na kwenda kuungana na mwendo kasi ya Mbagala.

Lakini pia awamu hiyo itahusisha barabara itakayokwenda Segerea.

Meneja Uhusiano wa Umma wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), William Gatambi alilileza Mwananchi jana kuwa hati za ununuzi ziko tayari na zimewasilishwa kwa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) bila pingamizi lolote kwa wafadhili.

“Usanifu wa kina wa miundombinu ya awamu ya tano umekamilika kwa hivyo, mara tu ADF itakapoidhinisha hati ya manunuzi, mchakato wa kupata mkandarasi utaanza,” alisema.

Alisema mjenzi atapatikana hivi karibuni na ujenzi utaanza Desemba mwaka huu, kwa sababu kazi kubwa za msingi zimekamilika.

‘‘Hadi sasa, kuna awamu sita zilizopangwa ambazo zitahudumia zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa jiji hilo na kwa sasa ni awamu ya kwanza pekee ndiyo inayofanya kazi,’’ alisema.

Awamu ya kwanza itahusisha barabara kutoka Kibaha Kimara kupitia Barabara za Mororogo, Kawawa na Mtaa wa Msimbazi na kuishia Kivukoni na Gerezani.

Akifafanua kuhusu BRT awamu ya pili, Mkurugenzi wa Fedha na Maendeleo ya Biashara wa Dart, Deusdelity Casmir alisema ujenzi huo umefikia asilimia 93, huku ukamilishaji wa miundombinu ndio suala pekee ambalo linasubiriwa.

“Mkandarasi anakamilisha uwekaji wa ‘scanner’ za nauli za getini ili kuruhusu wasafiri kutelezesha kadi zao juu ya scanner. Kama unavyojua, wateja watatumia kadi kupata usafiri wa mabasi yaendayo haraka,” alisema.

Casmir alisema Oktoba mwaka huu mkandarasi atakabidhi miundombinu ya awamu ya pili kwa Dart.

“Ujenzi wa mradi wa BRT ulipaswa kukamilika Machi mwaka huu lakini mkandarasi aliomba kuongeza mkataba kwa miezi kadhaa. Tuna matumaini miundombinu hiyo itakabidhiwa kwetu Oktoba ili kuwezesha mchakato wa huduma za BRT kuanza," alisema Casmir.

Kuhusu ujenzi wa awamu ya tatu ya mradi huo, alisema inaendelea kujengwa, huku makandarasi wakianza kujenga vituo vya abiria kuanzia madaraja ya juu ya makutano ya Chang’ombe na Mfugale.

Awamu hiyo inahusisha ujenzi wa miundombinu yenye urefu wa kilometa 23.6 kutoka Gerezani hadi Gongo la Mboto kupitia Barabara ya Nyerere.

Itahusisha pia katikati ya jiji na sehemu ya barabara ya Uhuru kutoka Kariakoo-Gerezani hadi Tazara.

Desemba mwaka jana, Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Edwin Mhede, alilieleza Mwananchi kuwa Benki ya Dunia (WB) ilitoa dola milioni 97.7 (Sh219 bilioni) kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya nne kati ya Tegeta kupitia Bagamoyo na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Bibi Titi katikati ya jiji.

Juni mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angela Kairuki, alisema Serikali inafanya mazungumzo na Mfuko wa Mazingira ya Kijani (GCF), ili kupata dola 260 milioni za Marekani (Sh648.7 bilioni) kwa ajili ya utekelezaji ya awamu ya sita ya mradi wa BRT.

Alisema lengo lilikuwa ni kuhakikisha awamu ya nne mpaka ya sita zinatekelezwa kwa wakati mmoja.

Alisema kwa sasa Serikali inafanya mazungumzo na GCF ili kupata uwezekano wa kutekeleza awamu hizo tatu kwa wakati mmoja hadi ifikapo 2025.

Awamu za ujenzi

Kwa sasa awamu za ujenzi wa mabasi hayo, unahusisha ujenzi wa mradi wa awamu ya tatu unaoendelea katika Barabara ya Nyerere hadi Gongo la Mboto, awamu ya nne ya Tegeta kupitia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Awali awamu ya pili ambayo imo mbioni kukamilika na kukabidhiwa inahusisha ujenzi wa barabara kati ya Mbagala na katikati ya jiji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live