Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi mkubwa wa maji Butiama, Musoma wasainiwa

46151aeaa1c036d8d1f35de3054e547b Mradi mkubwa wa maji Butiama, Musoma wasainiwa

Thu, 19 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Anthony Sanga amesema serikali kupitia wizara hiyo imeanza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuanza ujenzi wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mkoani Mara.

Sanga alisema hayo mkoani Mara juzi wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Maji wa Sh bilioni 70.5 wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika maeneo ya Musoma Vijijini na Butiama.

Mkataba huo ulisainiwa na Sanga na Mkandarasi Kampuni ya UNIK Construction Company ya Lesotho.

“Tupo hapa kutekeleza Ilani ya chama tawala cha CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 yenye kurasa 303 ambayo imetuelekeza kuhakikisha tunafikisha maji kwa wananchi wa Butiama na Musoma Vijijini kutoka Ziwa Victoria,” alisema Sanga.

Sanga alimshukuru Rais John Magufuli kwa kupeleka fedha za kutekeleza mradi huo kama alivyokuwa ameahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkoani humo.

“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Magufuli kwani mradi huu tunaosaini unatekelezwa kwa fedha za serikali yake,” alisema Katibu Mkuu.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi, alisema utajengwa kwa miezi 24, na kwa awamu ya kwanza utazalisha lita milioni 17 wakati mahitaji ya sasa ni lita milioni 12 kwa siku.

Awamu ya kwanza ya mradi itaanza kunufaisha vijiji 19 vya Butiama na Musoma Vijijini, lakini pia kijiji kimoja cha Wilaya ya Bunda.

Alitaja maeneo yakayonufaika na mradi kuwa ni miji ya Mugango, Kiabakari, Butiama na vijiji vya Kwibara, Nyamisisye, Singu, Mwanzaburiga, Kyawazaru, Kamugegi, Kyatungwe, Ryamugabo, Bumangi, Bisarye, Tiring'ati, Butiama, Rwamkoma, Buturu, Nyang'oma, Mayani, Katalyo na Tegeruka.

Sanga alibainisha kwamba eneo lenye mtandao wa majisafi litaongezeka kufikia asilimia 100 kwa miji ya Mugango, Kiabakari na Butiama na kwamba zaidi ya wakazi 165,000 watapata huduma ya maji kwa asilimia 100.

Sanga alibainisha kwamba lengo ni kuhakikisha zaidi ya vijiji 39 kutoka kwenye wilaya hizo vinanufaika pindi mradi utakapokamilika kwa asilimia 100, ambao kwa wakati huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita milioni 35 kwa siku.

Mradi unajengwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa wadau wa maendeleo Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (SFD).

Utiaji saini wa mradi huo mkubwa wa maji ni wa kwanza kutekelezwa tangu kuanza kwa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli.

Chanzo: habarileo.co.tz