Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpina azipa halmashauri nchini miezi sita

32067 Pic+mpina Waziri Mpina

Mon, 17 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Chato. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametoa miezi sita kwa halmashauri zote nchini Tanzania kukarabati majosho yasiyotumika, ikiwa hilo halitafanyika atazuia ukusanyaji wa ushuru kwenye idara ya mifugo.

Mpina ametoa agizo hilo jana Desemba 16, 2018 katika uzinduzi wa kampeni ya uogeshaji mifugo kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe iliyofanyika katika kijiji cha Buzirayombo wilayani Chato mkoani Geita.

Mpina amesema yapo majosho 2,428 nchi nzima lakini yanayofanya  kazi ni 1,409 tu, mengine 1,018 hayafanyi kazi na hakuna sababu za maana.

“Hayo majosho yote yakarabatiwe na yafanye kazi na halmashauri ambazo hazitakarabati hazitakusanya ushuru wa mifugo,” amesema.

Amewataka watendaji wa Serikali kusoma sheria na kuzielewa ili waweze kuzisimamia  badala ya kuvunja sheria nyingine kwa madai ya kusimamia sheria wanazofanyia kazi.

Waziri Mpina amesema  watendaji  wa Serikali wanaovunja sheria kwa madai ya kusimamia sheria nyingine watachukuliwa hatua ikiwemo kufungwa.

Katibu wa wafugaji Kanda ya Ziwa, Hamis Mashaka amesema ili kupambana na magonjwa ya mifugo Serikali inapaswa kuweka majosho maeneo ya karibu na mifugo kwa kuwa sasa mifugo mingi inaranda kutafuta malisho kutokana na ukosefu wa maeneo ya malisho.



Chanzo: mwananchi.co.tz