Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpigapicha wa Waziri Mkuu azikwa

MFINA.webp Mpigapicha wa Waziri Mkuu azikwa

Fri, 5 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKUU wa Wilaya ya Mwanga, Tom Apson, ameongoza mazishi ya aliyekuwa Mpigapicha wa Waziri Mkuu, Chris Mfinanga, yaliyofanyika kwenya kijiji cha Mangio, Vuchama, wilayani humo.

Akizungumza na waombolezaji kijijini hapo jana, Mkuu huyo wa Wilaya ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwira, alisema Mfinanga alikuwa mtu aliyejaa upendo ndiyo maana wengi wanahuzunishwa na kifo chake.

“Chris alikuwa mtu mcheshi na mwenye upendo, alisaidia wengi, lakini tusisahau Mungu ndiye mtoa riziki. Msikate tamaa kwa sababu Mungu yupo na alimwezesha Chris na ndiyo maana aliweza kuwasaidia wengine na hata kuwasomesha watoto wenu.”

“Ninawasihi muamini kuwa Yesu yupo na kwake kuna faraja. Amini Yesu yupo na usiamini katika mganga wa kienyeji au ushirikina. Tuache ramli, tumtegemee Mungu nasi tutapata faraja,” alisisitiza.

Akiongoza ibada hiyo, Mchungaji Kiongozi wa KKKT Usharika wa Vuchama, Bill Graham Msangi, aliwataka waombolezaji waweke mambo yao sawa na Mungu wao pamoja na majirani wanaoishi nao.

Akitoa mahubiri kutoka kitabu cha Ufunuo wa Yohana (14:13), Mchungaji Msangi alisema watu wanaomwamini Kristo wana heri kwa sababu wanapoaga dunia ni sawa na watu wanaoenda kupumzika baada ya taabu zao hapa duniani. “Wanaokufa katika Bwana wanaenda kupumzika baada ya taabu zao. Wana heri sababu matendo yao yanafuatana nao.”

“Neno la Mungu limesema; bali wao wasioamini, waongo wote, wachukiao na wezi wote na waabuduo sanamu, sehemu yao ni kwenye ziwa la moto ambao hata mende hawaungui. Hata uwe tajiri kiasi gani, au uwe mzuri kiasi gani au uwe baunsa, hautaweza kuzuia kuingia kwenye jehanamu ya moto eti kwa sababu ya ubaunsa wako.”

“Tunapaswa tujiandae kwa sababu siku ikifika, Mungu hataangalia uzuri ulionao. Yeye Mungu ni mzuri kuliko huo uzuri wako. Shetani alikuwa mzuri sana, lakini alipoasi alifukuzwa.”

Aliwasihi wafiwa na wakazi wa kijiji hicho hao wawe na umoja ili amani iweze kutawala. “Umoja ukae miongoni mwa familia, ukae miongoni mwa kaya nyingine na wanavijiji wote. Tukiishi kwa namna hiyo, amani itatawala kwa sehemu kubwa.”

Naye Padre Japhet Njaule wa Parokia ya Vuchama ambaye aliongoza mazishi ya baba yake Chris Mei 21, 2020, aliwataka waombolezaji wamtumaini Mungu na waishi kwa kujiandaa na kuwa tayari wakati wote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live