Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpango wa Jiji la Dodoma kuanza kwa uelimishaji

655e6bcf0c82837b39f213993601c03f Mpango wa Jiji la Dodoma kuanza kwa uelimishaji

Fri, 22 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inakaribia kuanza utekelezaji wa mpango kabambe wa jiji la Dodoma kwa kuelimisha wananchi wa kata za Mpunguzi na Matumbulu ili waweze kufanya maendeleo kwa kuzingatia mpango huo.

Timu ya wataalamu wa wizara hiyo pamoja na wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi, Imaculate Senje imeshakutana na wenyeviti wa mitaa iliyo kwenye kata hizo kuwajengea ufahamu kuhusiana na utekelezaji mpango huo.

Akizungumza na wenyeviti hao juzi katika ofisi ya Mtendaji Kata ya Matumbulu, Imaculate alisema wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeanza uhamasishaji wa utekelezaji wa mpango huo ili wananchi wauelewe na kuachana na dhana kuwa serikali inapora maeneo yao.

Kwa mujibu wa Imaculate, mpango huo kabambe utaanzia kata ya Mpunguni na kuhusisha maeneo ya mashamba na viwanda na baadaye katika maeneo ya makazi ya wananchi ambayo yatafanyiwa urasimishaji.

“Hapa tunataka tuepuke ujenzi holela katika maeneo hayo na kuzingatia mpango kabambe uliopo,'' alisema.

Alisema wakati wa utekelezaji wa mpango huo hatua ya awali, wataalamu watachukua taarifa za wamiliki wote kwenye maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya mashamba na viwanda ambayo yatapimwa na wamiliki wake kumilikishwa.

Alisema baada ya kumilika hatua hiyo, mtu hawataruhusiwa kufanya muendelezo wa maeneo hayo kinyume cha mpango huo kabambe.

Kwa upande wake, Ofisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aisha Masanja alisema lengo la kukutana na wenyeviti wa mitaa kabla ya kukutana na wananchi ni kuwataka kuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha kuhusu mpango huo.

“Inachotaka serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anabaki katika eneo lake na baada ya hapo itatolewa ramani ya msingi itakayoainisha shughuli ya kila eneo kulingana na mpango,” alisema.

Mpango kabambe wa jiji la Dodoma ulizinduliwa Februari mwaka 2020 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa ajili ya kulifanya jiji la Dodoma kuwa bora na la kisasa.

Chanzo: habarileo.co.tz