Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpango mpya wa malipo ya maji wahitimisha tatizo ulipaji wa madeni

18788 Pic+maji TanzaniaWeb

Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mkinga. Kuundwa kwa kamati za ufuatiliaji wa rasilimali za umma (Pets) katika sekta ya maji kwenye kata nne wilayani hapa, kumesaidia baadhi ya maeneo yaliyokuwa sugu kwa ukusanyaji wa mapato hayo kumaliza madeni yao.

Miongoni mwa waliomaliza madeni yao ni pamoja na kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Maramba wilayani hapa.

Hayo yalisemwa juzi wakati wa mdahalo ulioandaliwa na asasi ya Tanzania Women for Self Initiatives (Tawsei) wa kutathmini hali ya upatikanaji wa maji safi na salama wilayani Mkinga.

Wajumbe wa kamati za jumuiya za maji kutoka kata za Parungu, Kasera, Maramba, Bwiti na Moa waliozungumza katika mdahalo huo, walitoa ushuhuda wa hali ya ukusanyaji wa mapato ya maji ilivyokuwa ngumu kabla ya kuwapo kwa pets na mafanikio yanayopatikana hivi sasa.

Mweka Hazina wa Jumuiya ya Watumiaji wa Maji Kata ya Maramba, Rukia Said alisema sasa makusanyo yamefikia Sh1.8 milioni wakati zamani baadhi ya watumiaji walikuwa hawalipi.

“Lakini hawa wajumbe wa kamati ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali ya maji wametuelimisha na kutufanya tuwe na ujasiri wa kuingia hata kwenye kambi za majeshi na tukizungumza na uongozi unatuelewa, zamani tulikuwa hatuthubutu,” alisema Rukia.

Mhandisi msaidizi wa idara ya maji wilayani Mkinga, Castory Keneth alisema Jumuiya za Watumiaji wa Maji (Cowso), zipo kisheria na zina jukumu la kuishirikisha jamii kulinda vyanzo na miundombinu ya maji pamoja na kuchangia gharama za uendeshaji na upatikanaji wa maji.

Mkurugenzi wa Tawsei, Bernadeta Choma alisema awamu ya kwanza ya mradi huo ulisaidia kuundwa kwa kamati za ufuatiliaji wa rasilimali za umma katika sekta ya maji.

Pia, ulibaini kutokuwepo kwa mfumo imara wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na uchotaji wa maji kwenye mabomba.

Alisema ili kuhakikisha jumuiya zinatekeleza majukumu yake, wajumbe kutoka kamati za ufuatiliaji wa rasilimali za umma katika sekta ya maji kwenye maeneo yao wamekuwa wakitoa elimu ya faida ya kulinda vyanzo, miundombinu na kuchangia gharama ili upatikanaji wa huduma hiyo uwe endelevu.

“Taarifa tulizozisikia leo kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na jumuiya za watumiaji maji zinatupa faraja Tawsei na hata Foundation For Civil Society (wafadhili wa mdahalo) kwamba kuna mabadiliko na hii iwe chachu kwa jumuiya nyingine,” alisema Bernadeta.

Chanzo: mwananchi.co.tz