Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amesisitiza umuhimu wa kufanya tafiti za kina na kuunda mikakati madhubuti ili kubadilisha tabia na mazoea yasiyofaa yanayokwamisha maendeleo katika jamii ikiwemo wimbi la vijana wa kiume kupenda wanawake wenye umri mkubwa.
Ametoa wito huo alipokuwa akifungua Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 30 ya Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) katika Ukumbi wa Johari Rotana, Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mpango amebainisha baadhi ya tabia nyingine zinazofikirisha kuwa ni pamoja na kutojali muda, kukosa uaminifu kazini, na kutumia njia zisizofaa za kupata kipato. Pia ametaka ESRF na wataalamu wa fikra tunduizi (think tanks) kuangazia tabia zinazoibuka kama vijana kutumia muda mwingi vijiweni bila kazi, uchezaji kamari, utupaji ovyo wa taka, uchomaji moto ovyo wa nyasi na misitu, pamoja na ubinafsi.
Aidha, ameeleza umuhimu wa kuchunguza matumizi ya fedha kwa anasa badala ya kuweka akiba, ikiwemo matumizi makubwa kwenye sherehe kuliko kusaidia elimu na matibabu kwa familia zenye kipato cha chini.
Dkt. Mpango pia ameonya kuhusu kuongezeka kwa utegemezi na ukatili dhidi ya wanawake, watoto, na vitendo vya ushirikina kama mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Makamu amehimiza ESRF kufanya tafiti kuhusu changamoto za kimataifa kama mabadiliko ya teknolojia, uchumi usiohimili misukosuko, mizozo ya kisiasa, na mienendo ya soko la ajira ili kuandaa vijana kwa fursa zilizopo barani Afrika, hususan Tanzania.