Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpango: Tutaifungua Kigoma kibiashara

Aefaf1ba84526bb0d6be637ce23fbfd2 Mpango: Tutaifungua Kigoma kibiashara

Mon, 19 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema serikali imedhamiria kuimarisha miundombinu ya usafirishaji mkoani Kigoma ili kuufungua mkoa huo kibiashara kwa kuunganisha na mikoa mingine na nchi jirani.

Dk Mpango alisema hayo wilayani Kakonko, mkoani humo jana, akiwa kwenye siku ya mwisho ya ziara yake ya siku nne kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo ya wananchi.

Alisema mkoa wa Kigoma una fursa nyingi za kibiashara na nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, lakini pia biashara na mikoa mingine, lakini miundombinu duni ya kuunganisha na mikoa mingine na nchi jirani imekwaza wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa tija.

"Serikali imedhamiria kwa dhati kuhakikisha miradi ya barabara za kiwango cha lami kuunganisha na nchi jirani na mikoa mingine inakamilika katika kipindi kifupi kijacho, ujenzi wa meli mpya ziwa Tanganyika na uimarishaji wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma, yote ikilenga kuinua uchumi na shughuli za biashara kwa mkoa wa Kigoma," alisema Dk Mpango.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya barabara kwa mkoa huo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya alisema serikali inaendelea na mchakato wa kukamilisha barabara ya Kigoma hadi Tabora, eneo la Chagu wilaya ya Uvinza hadi Kazilambwa.

Alisema pia serikali inaendelea na mchakato kuhakikisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya kilometa 51 kutoka Uvinza hadi Daraja la Malagarasi unaanza Septemba, mwaka huu, huku utangazaji wa zabuni ukiendela kwa barabara kutoka Uvinza mkoani Kigoma kuelekea Mpanda mkoani wa Katavi.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais akiweka jiwe la msingi la Hospitali ya Wilaya Kakonko na kuitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inarudisha Sh milioni 137 ambazo zilirudishwa Hazina baada ya muda wa matumizi kwisha zikiwa hazijatumika ILI kutawezesha utekelezaji wa mradi huo kwenda kwa kasi.

Dk Mpango alisema serikali imedhamiria kuboresha utoaji huduma nchini kwa kuboresha majengo, vitendea kazi na watumishi ili huduma bora za afya ziweze kupatikana karibu na wananchi.

Awali, akitoa taarifa ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kakonko, Masumbuko Stephano alisema Sh bilioni 1.5 kinatarajia kutumika kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo na kwa kuanzia majengo saba yamejengwa kati ya majengo 32 yanayohitajika.

Alimuomba Makamu wa Rais kusaidia kurejeshwa kwa Sh milioni 187 zilizorudishwa Hazina kati ya Sh milioni 500 zilizotolewa awali kwa ajili ya mradi huo kutokana na kufungwa kwa mwaka wa fedha zikiwa hazijatumika.

Alisema hadi sasa Sh milioni 943.6 zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwa mwaka huu halmashauri imetenge Sh milioni 300 kukamilisha awamu ya kwanza na ya pili ya mradi huo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz