Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto wenye utata wateketeza mabweni Sekondari ya Ashira

59394 Pic+moto

Fri, 24 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Moto ambao chanzo chake bado hakijajulikana, umeteketeza mabweni mawili ya ghorofa ya shule kongwe ya Sekondari ya Wasichana ya Ashira, huku kiini cha moto huo kikiacha maswali mengi.

Utata unaojitokeza ni jinsi majengo mawili yasiyotegemeana kwa umeme kuungua kwa wakati mmoja.

Tukio hilo ambalo limesababisha uharibifu mkubwa wa vifaa vya wanafunzi na vingine vilivyokuwa kwenye mabweni hayo, lilitokea jana asubuhi wakati wanafunzi wakiwa madarasani.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira akizungumzia tukio hilo alisema, “hivi tunavyozungumza, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wako eneo la tukio na tathmini ya madhara itatolewa baada ya uchunguzi.”

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba aliliambia Mwananchi kuwa wanafunzi 73 wamepoteza vifaa vyao vyote ambavyo ni pamoja na mavazi.

Alisema kwa taarifa za awali, tukio hilo linaonyesha halijasababishwa na hitilafu ya umeme na kwamba uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo chake.

Pia Soma

“Tumefika eneo la tukio pamoja na watu wa uokoaji ila vifaa vya wanafunzi vimeungua vyote, kwa sasa tunajipanga tuone namna ya kuwasaidia, hasa ikizingatiwa eneo hili lina baridi,” alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wanafunzi hao hawatakosa mahali pa kulala kwa kuwa mabweni ya wanafunzi wa kidato cha sita yako wazi na wanachohitaji ni msaada wa vifaa na nguo.

Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa Marangu Mashariki, Exaud Mamuya alisema, tukio hilo limeacha maswali mengi kutokana na namna moto huo ulivyotokea kwa wakati mmoja.

“Mpaka sasa hakuna mwanafunzi aliyehojiwa, ili kujua chanzo cha moto huo, lakini ukiangalia ni mabweni mawili tofauti, kila moja liko eneo lake na hayashirikiani umeme,” alisema. “Sasa tunajiuliza, inakuwaje eneo ambalo halishirikiani umeme halafu yaungue moto kwa wakati mmoja?

“Bado maswali ni mengi ambayo tumeendelea kujiuliza kuhusiana na tukio hili, lakini tunasubiri taarifa ya uchunguzi ya vyombo vya ulinzi na usalama ili kubaini chanzo chake”

Alisema hakuna madhara ya kifo na kwamba tathmini ya mali zilizoteketea, inafanywa na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Moshi, ambayo ilifika eneo la tukio na Kikosi cha Zimamoto.

Mabweni hayo yalikuwa na uwezo wa kulaza wanafunzi zaidi ya 200.

Mkuu wa shule hiyo, Elizabeth Abdallah alipopigiwa simu kuzungumzia tukio hilo alisema hahitaji kuzungumza na mwandishi wa habari yoyote kuhusiana na tukio hilo.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Florah Temba na Fina Lyimo

Chanzo: mwananchi.co.tz