Moto mkubwa uliozuka usiku wa kuamkia leo Jumatano umeteketeza maduka sita Singida ambayo thamani yake haijafahamika bado.
Akizungumza na kituo kimoja cha radio mapema leo Agosti 16, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskasi Muragili amesema kuwa moto huo ulizuka saa 6 usiku kuamkia leo.
Muragili amesema mali zilizoungua ni pamoja na maduka yaliyokuwa na vifaa vya ujenzi, simu, nguo, stoo na mali nyingine katika maduka hayo ambayo yalikuwa katika jengo moja.
“Ni kweli moto ulikuwa ni mkubwa, ulianzia katika duka la kuuza nguo ambalo mwenye duka anasema kuwa kulikuwa na mali zenye thamani ya Sh60 milioni, lakini kwenye maduka ya simu na vifaa vingine hatujajua thamani yake,” ameeleza Muragili.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya, chanzo cha moto huo hakijafahamika licha ya taarifa kuwa ulianzia kwenye duka la nguo ambalo mmiliki alieleza kuwa alifunga saa 1: 30 jioni lakini moto ulianza kuwaka saa sita usiku.
Mkuu huyo amesema kuwa, taarifa zilitolewa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, vikosi hivyo vilifika eneo la tukio dakika 15 baadaye wakiwa na magari mawili ambao walifanikiwa kuuzima na kupunguza madhara katika maduka mengine.
Mmoja wa mashuhuda, Mary Mungaa amesema kazi iliyofanyika na Zimamoto imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kusambaa moto huo.