Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto waua watu 62, shule 44 zaungua

A316173ae4e9c1815fd16299ba4331d5 Moto waua watu 62, shule 44 zaungua

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JESHI la Zimamoto na Uokoaji limesema kati ya Januari hadi Desemba mwaka huu, moto umeua watu 62 katika matukio 1,925.

Mkaguzi wa Jeshi hilo, Joseph Mwasabeja alisema hayo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya shughuli ambazo jeshi hili limefanya kuanzia Januari hadi Desemba 30, 2020.

Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa katika muda huo, moto uliua wanaume 45, wanawake 17 na ulijeruhi watu 74 wakiwemo wanaume 52 na wanawake 22. “Kama mnavyojua hivi karibuni tumekuwa na matukio mengi ya kuungua kwa shule.

Shule zipatazo 44 zimeungua na kusababisha kupoteza maisha kwa baadhi ya wanafunzi, kuharibu miundombinu na kuteketea kwa vifaa vingi”ilisema jana.

Mwasabeja ilisema ili kupunguza majanga ya moto shuleni, jeshi limekubaliana na Chama Cha Skauti Tanzania kutoa elimu kwa wanafunzi baada ya wao kupatiwa mafunzo ya utoaji elimu ya kinga na tahadhari ya majanga ya moto.

“Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limebaini majanga mengi ya moto yanatokana na uzembe, hujuma na hitilafu za umeme”ilisema. Mwasabeja alisema jeshi hilo limeanzisha klabu rafiki za zimamoto katika shule za msingi na sekondari, na tayari wana klabu 786 zenye wanachama 34,018.

“Kwa upande wa shule za bweni tumebaini wanafunzi wanachaji simu kwa kificho kwa kutumia nyaya za umeme zilizopita darini, wanatumia heater na pasi bila kuwa waangalifu. Pia wabatumia mishumaa wakati umeme ukikatika na taa zinazotumia mafuta sehemu ambazo hakuna umeme”alisema.

Alisema jeshi limefanya uokoaji katika maeneo mbalimbali zikiwemo ajali za barabarani, mafuriko, kwenye migodi, mashimo ya vyoo, mito, mabwawa, baharini na maeneo mengine.

“Jumla ya uokozi 845 yalifanyika, matukio hayo ya uokozi yalisababisha vifo 495, kati ya hao wanaume ni 402 na wanawake 93”ilieleza taarifa hiyo. Alieleza kuwa kwenye uokoaji huo, kulikuwa na majeruhi 817 wakiwemo wanaume 570 na wanawake 247.

“Kwa huduma ya haraka juu ya majanga ya moto na maokozi Piga namba 114”ilieleza taarifa hiyo. Kuhusu mkakati wa kuongeza vitendea kazi katika mikoa na wilaya, Mwasabeja alisema Jeshi limeingia makubaliano na Shirika la Nyumbu kukarabati na kutengenezewa magari mapya ya kuzimia moto.

“Tunaishukuru serikali kupitia Rais John Magufuli imetupatia fedha katika bajeti iliyopita ya kununua magari matatu na katika bajeti hii tumetengewa tena bajeti ya magari matatu, tuna upungufu mkubwa wa mitambo (magari),”alisema na kuongeza: “Vifaa vya zimamoto na uokozi vinanunuliwa kwa gharama kubwa ambapo mtambo wa lita 500 unanunuliwa kwa takribani shilingi milioni 900, hivyo serikali inapotoa fedha kununua magari matatu inakuwa imetoa fedha nyingi” alisema.

Alisema tayari wamepeleka magari 13 katika Shirika la Nyumbu kwa jili ya ukarabati na wanatarajia kupokea magari matatu ya kwanza. Mwasabeja alitaja mkakati mwingine kuwa ni kuongeza kasi ya utoaji elimu ya kinga na tahadhari ya majanga ya moto kwa jamii. Pia watafanya ukaguzi kwenye maeneo yote ya mikusanyiko ya watu, shule za bweni na kutwa.

Chanzo: habarileo.co.tz