Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto waua mtoto wa miezi 20

Moto Waua Mtoto Mama wa mtoto aliyefariki akisaidiwa na wasamaria wema

Wed, 27 Mar 2024 Chanzo: Mwananchi

Mtoto wa mwaka mmoja na miezi nane amefariki dunia kwa kuungua na moto baada ya mama yake mzazi kumuacha ndani kukiwa na jiko la mkaa lenyewe moto.

Tukio hilo limetokea Machi 25, 2024 katika mtaa wa Igangidung'u uliopo Kata ya Kivavi halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe

Akizungumza Jana Machi 26, 2024 mama wa mtoto huyo Anna Mabiki (28) amesema alimuacha ndani akiwa amelala kwenye kochi na kwenda kupokea mafuta ya kupikia barabarani kwa dereva bodaboda ambaye hakupafahamu nyumbani kwake.

Amesema baada ya kuchukua hayo mafuta na kurudi nyumbani, ndipo alikutana na janga hilo la moto ambao uliondoa maisha ya mtoto wake huyo.

"Niliagiza mtu aniletee mafuta kule chini hapa kwangu hapafahamu akataka tukutane barabarani, lakini wakati ananikabidhi mafuta nageuka nyuma nyumbani kuna moto tukaanza kukimbia na yule kaka kuja kumuokoa mwanangu" amesema Anna.

Amesema alikuta nguo za mtoto wake zimeshika moto na kujaribu kumuinua ili kuokoa maisha yake bahati mbaya akaanguka watu waliokuwepo wakamwambia atoke nje ili wamsaidie kumtoa lakini bahati mbaya alikuwa tayari ameshafariki.

Balozi wa eneo la Uzunguni A katika mtaa wa Igangidung'u Grace Gadau amesema tukio hilo lilitokea usiku ambapo pamoja mtoto huyo kupoteza maisha vifaa vya nyumbani ikiwemo televisheni na kochi vimeteketea na moto.

"Mimi nilisikia yowe ile natoka nikakuta nyumba ya jirani moto unawaka nafika pale mtoto ndiyo wanampakia kwenye gari kumpeleka hospitali ila wanapofika hospitali yule mtoto hakupata hata dawa wakaambiwa tayari amefariki," amesema Grace.

Kufuatia tukio hilo Ofisa Mtendaji wa mtaa wa Igangidung'u Happines Sanga amewataka wazazi kuwa makini na watoto wao hasa kipindi hiki cha msimu wa baridi kwani mtoto anapokuwa karibu na moto unamsababishia hatari kubwa.

"Naomba wazazi tuwe makini na watoto hasa kipindi hiki cha msimu wa baridi, kwani mtoto anapokuwa karibu hivi na moto inamsababishia hatari kubwa sana" amesema Sanga.

Mkuu wa upelelezi wilaya ya kipolisi Makambako, Gotfrid Kimboy amewataka wananchi kuacha tabia ya kulala na majiko ya mkaa ndani ili kuepuka vifo ambavyo vinaweza kuzuilika.

Amesema jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo cha mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi nane.

"Ni kweli huku kuna baridi ni sawa lakini lazima tuwe makini kwa sababu haya majiko ya mkaa tunayoweka ndani hata kama ni mtu mzima mkaa unatoa hewa ya sumu hivyo utakosa hewa na utakufa" amesema Kimboy.

Baadhi ya majirani wa mtaa huo akiwemo Julius Kiowi amesema mara baada ya kutokea kwa janga hilo la moto walijitoa ili kumsaidia mtoto huyo kwa kumtoa nje na kueleza kuwa mama wa mtoto huyo pia amejeruhiwa kwa moto usoni na mikononi.

"Nilitoka nje nikakuta watu nikasogea eneo la tukio mmoja wetu aliingia chini na kumvuta mtoto kisha kutoka naye nje" amesema Kiowi.

Chanzo: Mwananchi