Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto wateketeza vibanda 200 Morogoro

Moto Sokooo Moto wateketeza vibanda 200 Morogoro

Thu, 13 Oct 2022 Chanzo: Global Publishers

Moto mkubwa umeteketeza bidhaa pamoja na vibanda vya wafanyabiashara zaidi ya 200 wa soko la Ruaha Mikumi mkoani Morogoro.

Akizungumza jana Oktoba 12, Mwenyekiti wa soko hilo, Ebu Lipenege amesema mbali ya bidhaa kuungua, pia baadhi ya wafanyabiasha wameibiwa bidhaa zao na watu waliokuwa wakivunja maduka na kuondoka na bidhaa.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa soko hilo lilianza kuungua moto saa 3 usiku, lakini haikuwezekana kuuzima kutokana na udhaifu wa vifaa vya kuzimia moto, huku gari la Zima moto likishindwa kufika kwenye chanzo cha moto.

"Kwa sasa hatuwezi kujua moto huu umesababisha hasara kiasi gani, maana baadhi ya maeneo bado unawaka na tunaendelea kuuzima, lakini kwa tathimini ya haraka ni hasara kubwa imewakumba wafanyabiasha hawa," amesema Lipenege.

Kwa upande wake Diwani wa kata Ruaha, Alex Gwila amewataka wafanyabiasha hao kuwa na moyo wa subira na uvumilivu wakati wataalamu wakiendelea kuchunguza tukio hilo.

"Madhara yamekuwa makubwa kwa sababu hili tukio limetokea usiku, kwa hiyo wafanyabiasha waliounguliwa bidhaa zao na wengine walioibiwa wawe wavumilivu wakati suala hili linachunguzwa.

"Jeshi la Zima Moto lilifika japokuwa walikuta moto umeshika kasi na umeshateketeza sehemu kubwa ya soko lakini tunajua ni kutokana na umbali kutoka Mikumi hadi Ruaha ni zaidi ya kilometa 35," amesema Gwila.

Kufuatia tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaji Majid Mwanga ameunda kamati maalumu inayowajumuisha wataalamu kutoka jeshi la zima moto na jeshi la Polisi kuchunguza tukio hilo ili kujua chanzo cha moto na hasara kiasi gani imetokana na moto huo.

"Kamati niliyoiunda tayari imeshafika pale kwenye eneo la tukio na imeshaanza kazi naamini itafanya uchunguzi vizuri ili kama Serikali tujue nini cha kufanya ili kuepuka majanga mengine kama haya yasitokee," amesema Alhaji Mwanga.

Chanzo: Global Publishers