Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto wateketeza maduka saba jengo la UWT

UWT Maduka Moto wateketeza maduka saba jengo la UWT

Tue, 6 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Maduka saba katika Jengo la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Shinyanga yameteketea kwa moto.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara wa Mtaa wa Mjini lilipotokea tukio hilo, maduka hayo ni ya nguo, vifaa vya kuandikia (stationery), nafaka na mahitaji ya nyumbani.

Wafanyabiashara hao wamesema walipata taarifa moto ulianza kuwaka saa 9 usiku wakuamkia leo Juni 6, 2023, walipofika eneo la tukio saa 10 alfajiri tayari mali zote zilikuwa zimeteketea.

Mmoja wa Wafanyabiashara hao, Edward Flavianus amesema alipofika eneo la tukio hakufanikiwa kuokoa mali yoyote sababu vitu vyote vyenye thamani ya Sh20 milioni vilikuwa vimeungua moto.

“Nilipigiwa simu saa 10 alfajiri nilipofika hapa eneo la tukio nilikuta mali zangu zote zimeteketea kwa moto hakuna ambacho tumefanikiwa kuokoa na moto huu inaonyesha ulianza kuwaka majira ya saa 8 usiku,”amesema Flavianus

Baadhi ya wafanyabiashara ambao maduka yao hayakuteketea moto wamepongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kufika kwa wakati eneo la tukio na kudhibiti moto huo usiteketeze maduka yote.

Katibu wa UWT mkoani Shinyanga, Asha Kitandala amesema tukio hilo limewarudisha nyuma wafanyabiashara waliokuwa wakifanyia biashara katika jengo hilo na kwamba UWT walikuwa wakilitegemea kwa mapato.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, Mrakibu Martin Nyambala amesema jeshi hilo lilipata taarifa saa 9 usiku, walipofika eneo la tukio walifanikiwa kuzima moto kwenye maduka sita lakini saba yaliteketea.

“Chanzo cha Moto huu bado kina chunguzwa, lakini tunatoa wito kwa wafanyabiashara wawe na vizimia moto kwenye maduka yao, pamoja na kutoa taarifa mapema hasa kwa walinzi wanapoona matukio ya moto wasipige simu kwanza kwa mabosi wao, bali wapige kwa Jeshi la Zimamoto kwa namba 114,”amesema Nyambala

Chanzo: Mwananchi