Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto wateketeza duka Bukoba, hofu yatanda

Bukoba Moto Hofu Moto wateketeza duka Bukoba, hofu yatanda

Tue, 1 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Moto ambao haijafahamika chanzo chake, umesababisha taharuki kwa wakazi wa Kata ya Miembeni, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera baada kuwaka kwenye chumba cha duka kilichokuwa na magodoro pamoja na bidhaa nyingine.

Moto huo ulianza jana usiku Oktoba 31 muda wa saa 1:30 jioni na haukuleta madhara kwa wakazi jirani na eneo hilo, lakini umeunguza magodoro na bidhaa nyingine ambazo thamani yake haijajulikana.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera, Zabrone Muhumha amesema kupitia namba yao ya dharula 114, walipata taarifa ya moto huo na hivyo kuchukua hatua haraka na kufika eneo la tukio.

Amesema baada ya muda mfupi walianza kudhibiti moto huo kwa kutumia magari yao ya zimamoto moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba na jingine kwenye kituo chao cha Zimamoto na Uokoaji Bukoba.

"Baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi kupitia namba yetu ya dharula 114 tulifika eneo la tukio na kuanza kuudhibiti moto na hatimaye tulifanikuwa kuuzima kabla haujaleta madhara makubwa," amesema Kamanda Muhumha.

Amesema wataendelea kutoa taarifa zaidi baada ya kuzungumza na wenye maduka ili kujua ni hasara kiasi gani imetokea.

Mmoja wa mashuhuda Jamal Ramadhani amesema, muda wa usiku alishuhudia moto mkubwa ukiwaka kutokea kwenye duka moja linalouza magodoro na baada ya muda mfupi magari ya zimamoto yalifika na kuanza kuuzima ingawa bidhaa ndani ya duka zilikuwa zimeshateketea.

Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Kagera, Samweli Mandali amesema baada ya moto huo kutokea walichukua hatua za kukata umeme ili kama moto huo umetokana na hitilafu ya umeme usiweze kuleta madhara makubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live