Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto shule ya Ashira hujuma

59742 Pic+ashira

Sun, 26 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Tamisemi, Suleman Jaffo amesema tukio la moto katika Shule ya Sekondari ya wasichana Ashira mjini hapa limesababishwa na hujuma.

Kufuatilia hali hiyo, waziri huyo amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina na kwa haraka kuwabaini waliohusika na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Jafo alisema hayo jana alipotembelea shule hiyo na kujionea hali halisi ya uharibifu uliotokana na tukio hilo lililosababisha mabweni wawili kuungua na mali zilizokuwemo ikiwamo vitanda  na vitu vingine vya wanafunzi kuteketea moto.

Tukio la moto katika shule hiyo lilitokea Mei 23 majira ya asubuhi na kuunguza mabweni mawili na vibanda na mali za wanafunzi 73.

 “Tukio hilo la moto halikusababishwa na umeme, inaonekana ni  hujuma ya makusudi. Kuna mtu au watu wenye nia mbaya na wanafunzi wa Ashira.”

“Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viendelee kuchunguza, wote waliofanya hivyo wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Aidha, Jaffo alisema kutokana na tukio hilo, wataalamu kutoka ofisi yake watafika katika shule hiyo leo ili kufanya tathmini na kutoa taarifa nini ambacho kinapaswa kufanywa katika mabweni hayo.

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Ave Maria Semakafu ambaye alifika shuleni hapo mapema kabla ya Jaffo na kuondoka naye alisema kulingana na mazingira ya tukio hilo inaonyesha ni hujuma.

Alisema shule hiyo kwa sasa inachukua wasichana 600, lakini itakapofanyiwa ukarabati itachukua wanafunzi 1,000 ili itusaidie kuongeza hamasa kwa watoto wa kike kupata elimu.

Chanzo: mwananchi.co.tz