Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto ‘kichaa’ tishio kwa misitu Iringa

Motopic Moto ‘kichaa’ tishio kwa misitu Iringa

Wed, 17 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Moto kichaa kwenye mashamba ya miti katika wilaya za Mkoa wa Iringa umetajwa kuwa tishio kubwa kwa wawekezaji na wakulima.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kongamano la uwekezaji kwenye sekta ya misitu mkoani Iringa, baadhi ya wakulima wa mazao ya misitu na wawekezaji wamesema karibu kila siku kuna msitu unawaka moto huku kukiwa hakuna vifaa vya uzimaji.

Wakati hoja hiyo ikizungumzwa, moto mkubwa umeteketeza zaidi ya heka 100 katika msitu ulio kwenye kata ya Ukumbi wilayani Kilolo.

Mkulima wa miti kutoka kijiji cha Masalali kata ya Ukumbi wilayani Kilolo, Tendo Mgidange amesema hawakuwa na vifaa vya uzimaji jambo lililosambabisha zaidi ya heka 1000 kuteketea.

Mshauri wa wavunaji wa miti na mkulima wa Wilaya ya Mufindi, Godfrey Mosha amesema zaidi ya heka 100 zimeungua mwezi uliopita na kumsababishia hasara kubwa.

“Hali hii ni mbaya jamani na inatishia uwekezaji naomba chonde tusiifumbie macho, tuchukue hatua haraka sana, juzi juzi nimepoteza miti mingi sana,” amesema Mosha.

Mkurugenzi wa kampuni ya Qwihaya, Lenard Mahenda amesema inahitajika hatua za haraka kudhibiti moto huo ili kuokoa misitu mingi iliyopandwa kwa gharama.

Mbunge wa Mufindi, Cosato Chumi amewashauri wamiliki wa miti kujenga uhusiano mzuri baina yao na wanavijiji ili iwe rahisi kusaidia uzimaji, moto unapoanza.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Saad Mtambule alikiri kuwa moto ni tatizo kubwa na katika kipindi kifupi alichokaa kwenye wilaya hiyo zaidi ya hekta 7,000 zimeteketea kwa moto.

“Sababu kubwa ni uandaaji wa mashamba, uwepo wa madalali na usimamizi mdogo hata hivyo tumeshaanza kufanyia kazi, tumeandaa mashindano ya kuzuia moto ili wanavijiji wawe walinzi wa kwanz,” amesema.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Damas Ndumbaro ameziagiza kamati za ulinzi na usalama kuwachukulia hatua watakaobainika kufanya hivyo kwa sababu ni kosa la jinai kuchoma moyo.

Amesema sheria inaonyesha kuwa atakayebainika kufanya kosa hilo atafungwa miaka 14, hivyo ikiwa itatekelezwa kwa vitendo itapunguza madhara ya moto.

Chanzo: mwananchidigital