Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto Mlima Kilimanjaro bado kuathiri utalii

699e46684fda3b7628ea739ab09a1a45.png Moto Mlima Kilimanjaro bado kuathiri utalii

Tue, 13 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MOTO katika eneo la mapumziko kwa watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro la Whona haujaathiri shughuli za utalii, wakiwamo wageni wanaopanda mlima huo wenye urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari.

Hadi jana timu ikihusisha vikosi vya zimamoto, wananchi wa vijiji jirani na mlima huo, na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, walikuwa eneo la tukio wakikabiliana na moto huo.

Kamishina Msaidizi Mwandamizi, Idara ya Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Pascal Shelutete, alisema jana kuwa bado moto ulikuwa unaendelea kuwaka.

Aliyasema hayo wakati akitoa taarifa kabla ya timu ya wanahabari na wataalamu kwenda eneo unapowaka moto huo.

“Moto ulianza kuzimwa jana usiku lakini kutokana na upepo mkali ulituzidi nguvu...pamoja na hali hiyo niwatoe hofu wageni wetu kwamba tunachukua tahadhari zote za kiusalama bila kuathiri shughuli za utalii,” alisema Shelutete.

Alisema ilitarajiwa moto huo ungeathiri kwa kiwango kikubwa wageni wanaopanda mlima huo kupitia lango la Marangu, lakini hali ni tofauti, wageni wanaendelea kupanda na tahadhari za usalama zinachukuliwa.

“Kimsingi bado moto unaendelea kuwaka kwa kasi lakini tunaamini timu ya watu ikiongozwa na wataalamu na wanafunzi wa Chuo cha Mweka watapata mafanikio,” alisema Shelutete.

Alisema Whona ni kituo cha kupumzika wageni wanaotumia njia ya Mandara na Horombo na kwamba Tanapa inaamini kwamba moto huo utadhibitiwa.

Shelutete alisema chanzo cha moto hakijafahamika, na uchunguzi unaendelea na kwamba Tanapa inaendelea kuchukua tahadhari kwa lengo la kuhakikisha usalama wa wageni na mali zao unaimarika.

Kilele cha Kibo chenye urefu wa mita 5,895 sawa na futi 19,340, ni kivutio kikubwa kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi kwa sababu ya kufunikwa na theluji mwaka mzima.

Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro ina ukubwa wa kilometa za mraba 755 na iko umbali wa kilometa 45 kutoka Moshi Mjini, kusini mwa Mkoa wa Kilimanjaro, 2 ° 50'-3 ° 10'S latitude, 37 ° 10'-37 ° 40'E longitude.

Chanzo: habarileo.co.tz