Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moro kumkumbuka JPM kwa daraja la Kilombero

0791f5e7d0f8cffdb6a1a262db14e03e Moro kumkumbuka JPM kwa daraja la Kilombero

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANANCHI wa Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi mkoani Morogoro wamemtaja Rais John Magufuli kuwa ni mkombozi wao kutokana na kujengewa daraja kubwa la kisasa la Mto Kilombero.

Baadhi ya wananchi wa Ifakara kwa nyakati tofauti wameikumbuka Mei 5, mwaka 2018 ilikuwa ni siku ya muhimu kwa wakazi wa wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga pale Rais Magufuli alipozindua rasmi daraja hilo liliopewa jina la Magufuli.

Wakazi hao waliojitambulisha kwa majina ya Amina Shaaban pamoja na Peter Michael licha ya kuonesha masikitiko kutokana na kifo hicho, walimtaja ni mkombozi wa wananchi wa wilaya hizo kwa kujengewa daraja la mto Kilombero .

Shaaban alisema watamkumbuka kwa utendaji wake uliotukuta na kusimamia utendaji wa serikali yake inayowajali watu wanyonge na uwajibikaji.

"Tupo na majonzi makubwa sisi wananchi wa Ifakara na hii inatokana na jinsi alivyowezesha ujenzi wa daraja hilo ambapo kwa sasa wananchi wa maeneo haya tunauona mwanga wa maendeleo kwani kikwazo chetu cha maendeleo kinaondoshwa kwa kujengewa daraja,"alisema Amina.

Wakazi hao walisema kipindi cha uzinduzi wa daraja hilo watu walilia machozi ya furaha huku wakikumbuka vifo vya watu 30 kivuko cha Kilombero kilipozama kabla ya kuanza kwa ujenzi wake mwaka 2014.

Pia walieleza kuwa wapo watu waliopoteza maisha nyakati kivuko kikiharibika na magari kushindwa kuvushwa kutoka upande mmoja kwenda mwingine ambao wengi wakiwa ni wagonjwa waliokuwa wanapelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Francis ya Ifakara.

Baada ya uzinduzi wa daraja hilo lenye urefu wa meta 384 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 9.1 Rais Magufuli aliwasisistiza wananchi utunzaji wa miundombinu ya daraja hilo ili liweze kudumu kwa muda mrefu.

Pamoja na hayo aliwaeleza kuwa hiyo ni fursa kwao ya kusafirisha mazao na bidhaa nyingine kwa ajili ya biashara zinazotoka na kuingia katika wilaya zinazonufaika na uwepo wa daraja hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz