Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Monsinyori Msimbe ataka jamii kuwaenzi wazee

8e5718b86d625677abe6bc8fec746a00 Monsinyori Msimbe ataka jamii kuwaenzi wazee

Sun, 21 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MSIMAMIZI wa Kitume Jimbo Katoliki Morogoro, Monsinyori Lazarus Msimbe ameitaka jamii kuwaenzi wazee ambao huchochea muunganiko wa desturi na mila zilizo njema.

Amesema wazee ni maktaba za mila, tamaduni na desturi husika katika jamii.

Aliyasema hayo kwenye sherehe ya watawa iliyofanyika Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan mkoani Morogoro, iliyowakutanisha watawa wa kike na wa kiume, wanaofanya utume wao katika jimbo la Morogoro

Monsinyori Msimbe alisema kuwa kila jamii inawahitaji wazee ili kuelekeza mila na desturi njema katika mashirika na jamii, hivyo kuna umuhimu wa kuwaenzi na kuwasikiliza wazee na hasa katika mema wanayoweza kutolea ushauri au kuelekeza katika kujenga maadili ya taifa na jamii.

Alisema kuwa jamii isiyo na wazee ni jamii isiyo na historia kwa sababu wazee ni maktaba za mila na tamaduni.

Alisema kuwa wazee ni baraka na hazina katika jamii au mashirika mbalimbali, hivyo wapewe nafasi kutumia busara zao kushauri mambo mema kadiri inavyowezekana

Msimbe alieleza kuwa ziko baadhi ya jumuiya za watawa, zinazowadharau wazee na kudai wanasumbua na wamepitwa na wakati. Alishauri jumuiya za watawa kuacha tabia hiyo ya kuwaona wazee hawana faida kwao.

“Si vyema kuwadharau wazee wetu, twende nao taratibu, najua sisi vijana spidi yetu ni kubwa lakini tukiendelea na spidi hiyo tutawaacha wazee nyuma na pengine tutapotea huko tunakokimbilia, tuwaenzi wazee na tuwaheshimu,” alisema.

Monsinyori Msimbe aliitaka jamii na mashirika mbalimbali ya kitawa, kutambua mchango wa wazee kwa kuiga mfano wa Simeoni na Anna, ambao kwa pamoja waliifurahia siku yao ya wokovu, baada ya kukutana na Yesu ambaye ni utimilifu wa matumaini na maisha ya kila mwanadamu.

Chanzo: habarileo.co.tz