Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mnyeti kumweka ndani mwenyekiti CCM ikiwa...

18077 Pic+mnyeti TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Simanjiro. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula kuhakikisha Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Awadhi Omary anakamatwa na polisi na kulazwa mahabusu endapo ataendelea kusababisha migogoro ya ardhi kwenye kitongoji cha Sukuro.

Mnyeti alitoa agizo hilo jana wakati akitatua mgogoro wa ardhi wa miaka 10 wa kugombea kitongoji cha Kitiangare Kati, Kijiji cha Sukuro na Katikati.

Mnyeti akizungumza mbele ya Chaula na Omary, alimuonya mwenyekiti huyo kutokuwa kitovu cha kusababisha migogoro ya ardhi isiyo na tija.

Alisema awali, alipata taarifa kuwa mwenyekiti huyo alifika siku moja kabla yake na kufanya kikao na wananchi wa Kitiangare na kuwashawishi wakatae kwenda Kijiji cha Sukuro na wabaki Kijiji cha Katikati.

Awali, akizungumza na wananchi wa Katikati, Mnyeti aliwashukuru kwa uvumilivu, busara na hekima walizozitumia katika kupigania haki ya kitongoji chao.

“Ni zaidi ya miaka 10 sasa mgogoro huu wa ardhi umekuwa ni kero hii ni kutokana na siasa zisizoleta maendeleo hivyo kuwafanya wananchi kushindwa kuendelea kujikwamua kiuchumi na haya ni majibu kutoka serikali kuu kitongoji cha Katikati kibaki katika kijiji cha Sukuro,” alisema Mnyeti.

Hata hivyo, Omary alikanusha kusababisha mgogoro kwenye eneo hilo akisema amekuwa msuluhishi na si mchonganishi.

“Mkuu wa mkoa amepewa taarifa potofu juu ya hilo, wilaya hii kuna baadhi ya viongozi wasio waaminifu na wametumia fursa hiyo kutoa maelezo yasiyo ya kweli,” alisema Omary.

Mmoja kati ya wananchi wa eneo hilo, Abraham Koringo alipongeza uamuzi huo akisema baadhi ya viongozi walitumika kusababisha mgogoro huo uliodumu kwa miaka 10 pasi na sababu.

Mgogoro huo uliwahi kusababisha ugomvi kati ya aliyekuwa mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Henry Shekifu.

Chanzo: mwananchi.co.tz