Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mnyeti atangaza vita kwa wanaokwamisha viwanda

9701 Mnyeti+pic TZWeb

Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ametangaza vita dhidi ya wanasiasa uchwara wanaokwamisha uanzishwaji wa viwanda ndani ya mkoa huo na atawachukulia hatua kali. 

Mnyeti ameyasema hayo leo Juni 21, mjini Babati wakati akizungumza kwenye kikao cha wadau wa maendeleo kujadili mambo ya uwekezaji ndani ya mkoa huo. 

Amesema hayuko tayari kuona maendeleo yanarudishwa nyuma mkoani kwake na wanasiasa wachache wenye kulenga siasa chafu za majitaka, badala ya kutanguliza mbele uzalendo na maendeleo ya Taifa.

"Sitamuonea haya mwanasiasa uchwara kuna viwanda vingi vilikuwa vinaanzishwa, ila kutokana na masilahi ya wanasiasa uchwara vilikwama na kuanzishwa mikoa ya jirani, nitapambana na wanasiasa wa aina hiyo," amesema Mnyeti. 

Ametoa mfano wa kiwanda cha alizeti kilichokuwa kijengwe eneo la Sigino mjini Babati, lakini kutokana na siasa chafu kikaenda kujengwa mkoa jirani wa Singida hivyo mkoa wa Manyara ukakosa fursa hiyo. 

Amesema kutokana na nia thabiti ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na viwanda vingi ili kutengeneza fursa za ajira na kukuza uchumi, yupo tayari kupigiwa simu hata usiku wa manane. 

"Kama ni suala la uanzishwaji wa viwanda kwa hapa mkoani Manyara, hata usiku wa manane wewe piga simu kwangu nami nitakupa ushirikiano wa kutosha tuje tufanye kazi kwa masilahi mapana ya nchi yetu," amesema Mnyeti. 

Amesema hadi sasa mkoa huo umefanikiwa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati 68 na wanatarajia hadi mwezi Desemba watakuwa wamefanikiwa kuwa na viwanda 100. 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz