Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Mnapoajiri mtupe pia  kipaumbele walemavu’

A586eb2762d435fe682975b28eaedc0d.png ‘Mnapoajiri mtupe pia  kipaumbele walemavu’

Mon, 5 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

ULEMAVU ni hali ya mtu kuwa na hitilafu ya kudumu ya mwili au akili kulinganisha na watu wengine. Ingawa walemavu wengi wana uwezo wa kufanya mengi kama watu wengine, lakini wakati mwingine hali zao huweza kuwawekea mipaka au vikwazo wasiweze kutekeleza shughuli fulani katika maisha yao kulinganisha na wasio na ulemavu.

Watu wenye ulemavu wamegawanyika katika makundi tofauti kulingana na hali ya ulemavu wao. Kuna wenye ulemavu wa viungo kama miguu na mikono, ulemavu wa kusikia, kuona, kunusa, ulemavu wa akili na mfumo wa fahamu au ulemavu wa ngozi.

Licha ya ulemavu wao, bado watu hawa wana haki ya kupata mahitaji kama ilivyo kwa watu wengine kwa maana ya elimu (kusoma), kupata chakula, kulindwa usalama wao, huduma bora za afya, kuheshimiwa, kutobaguliwa na haki ya ajira ili kujipatia kipato.

Sera ya taifa ya maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu na Sheria Namba 2 ya Ajira kwa Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 1982 inamtaka kila mwajiri kuhakikisha anaajiri asilimia mbili ya watu wenye ulemau katika taasisi au kampuni yake. Yaani, kama kampuni ina wafanyakazi 100 basi angalau wawili wawe walemavu. Je, ni kiasi gani hili linasimamiwa na kutekelezwa?

Na katika Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa kimataifa, ibara ya 27 (e, g, h, i, j) inagusa masuala ya kazi na ajira mkwa walemavu, ikisisitiza kwamba watu wenye ulemavu wana haki ya kufanya kazi sawa na watu wengine.

Baadhi ya yaayotajwa na ibara hiyo ni kuondoa ubaguzi kwa misingi ya ulemavu katika maeneo yote ya ajira ikiwa ni pamoja na katika hali ya kutafuta kazi, kuajiriwa kuendelea na ajira, kupandishwa cheo

kazini na kufanya kazi katika mazingira salama kiafya.

Pia inazungumzia kulinda ajira za watu wenye ulemavu kuhusu usawa katika malipo ya ujira kwa kazi ile ile, usawa wa fursa, usalama kazini na uwezo wa kutoa malalamiko na kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaweza kujiunga pamoja na kuingia kwenye vyama vya wafanyakazi sawa na mtu mwingine yeyote

Wakati wa maadhimsiho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanywa Machi 8 mwaka huu, yalikuwa na kaulimbiu ya ‘Wanawake katika uongozi, chachu kufikia dunia yenye usawa.’

Hii ni siku ambayo dunia hukaa chini kwa maana ya makundi ya watu mbalimbali, mashirika, taasisi na wadau wa maendeleo kuangalia pia kutafakari namna ya kumnyanyua mwanamke ambaye kwa muda mrefu amekuwa akikandamizwa na mifumo mbalimbali duniani.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, wadau wanaosimamia makundi ya walemavu, vijana na wanawake walianzisha mradi wa ‘Kijana Wajibika’ kupitia Shirika la Restless Development unaolenga kumjengea uwezo kijana kwenye masuala mazima ya uongozi.

Kupitia mradi huo kijana anatazamiwa kuwezeshwa katika kutambua nafasi yake na hivyo kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo.

Hatua hiyo pia inajielekeza kwenye lengo namba 16 la Maendeleo Endelevu linalolenga kuendeleza jamii jumuishi na yenye amani kwa ajili ya maendeleo endelevu, kutoa haki kwa wote na kujenga taasisi imara zenye kuwajibika katika nyanja zote.

Lengo hili linahamasisha jami kuhakikisha kunakuwepo usawa na ushiriki sawa wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kutokana na makundi haya kutengwa mara kwa mwara katika ushiriki wa masuala mbalimbali ya maendeleo.

Makundi haya pia hutengwa katika msuala ya uongozi na ushiriki sawa katika vyombo vya maamuzi kuanzia kwenye familia, kwenye taasisi mbalimbali hadi kwenye uongozi wa jamii na hasa wa kisiasa.

Clara Mchunguzi, ofisa mradi kutoka Shirika la Restless Development, anasema kuwa ipo mikakati mingi imewekwa kwa ajili ya kutetea haki za watu wenye ulemavu lakini kwa hali halisi si watu wengi wamekuwa makini kuzingatia haki zao ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya jamii katika kuleta maendeleo.

“Tupo katika mikoa 18 nchini, tunashirikiana na taasisi ndogondogo za mikoani katika kuendelea kuwajengea uwezo jinsi gani kuna ushiriki na ushirikishwaji wa wanawake na watu wenye ulemeavu kwa kumlenga mtoto wa kike. Lengo ni kufikia asilimia 40 kwa 60 huku 60 wakiwa ni wanawake na 40 wanaume na wale tutakaowafikia, asilimia tatu ni watu wenye ulemavu lakini tukimlenga msichana zaidi,” anasema Clara.

Kutokana na vijana wengi wenye ulemavu kubaguliwa na jamii, Clara anasema wanalenga kufawanya waseme vipaumbele vyao ili serikali iweze kusikia na kuona ni kwa namana gani wanaweza kusaidiwa.

“Kama shirika tayari tunao vijana wa kujitolea kwenye mikoa yote 18. Miongoni mwao wapo wenye ulemavu ambao ni vijana watatu walioko kwenye mikoa mitatu tofauti na wote ni wa kike na wanafanya vizuri. Hawa wanasaidia pia kuhamasisha vijana wengine kushiriki kikamilifu kwenye mradi wa kijana wajibika,” anasema Clara.

Anasema kila shirika au taasisi wanayoshirikiana nayo wamekuwa na sera zao kulingana na majukumu yao lakini bado wanasimamia malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs)

“Kutokana na uzoefu wa kazi tunayofanya na mashirika mbalimbali, si mashirika mengi ambayo yamekuwa yakitoa kipaumble kwa watu wenye ulemavu hivyo kama sera haisemi basi kuna haja ya wadau kwenye mashirika tunapofanya shughuli zetu tuwashirikishe kikamilifu watu wenye ulemavu. Kama wanao uwezo wapewe nafasi na kama matangazo ya kazi yakitolewa hawaombi, basi tuwe na jitihada za makusudi za kuwatafuta,” anasema.

Anasema wakati mwingine kushindwa kujitokeza kwao ni kutokana na mazingira ya ukatili na ubaguzi dhidi yao yaliyojengeka kwa muda mrefu katika jamii zetu.

Decarisa Mmari, msichana mwenye ulemavu ambaye amepewa nafasi ya kujitolea kufanya kazi katika Shirika la Restless Development anasema kutokana na ulemavu wake anajaribu kutumia fursa zinazopatikana katika jamii ili ajikomboe na kufikia malengo yake ya kujitegemea.

Akizungumza siku ya wanawake, Decarisa anasema kutokana na kaulimbiu ya mwaka huu ili kufikia dunia yenye usawa wa kijinsia ni muhimu kuyatilia maanani makundi matatu (wanawake, vijana na walemavu) kwa maana ya kuyajumuisha kwenye ngazi ya maamuzi.

Anasema makundi hayo yanapaswa kujumuishwa kuanzia nyumbani, kwenye ngazi ya serikali za mitaa na hadi taifa na kwamba wakati bado dunia inapigania wanawake kufikia usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50, zipo changamoto nyingi wanazopitia wanawake wenye ulemavu ikiwemo ya ajira ili waweze kujikimu.

“Mimi kama nakutana na changamoto mbili; kwanza kama mwanamke pili kama mwanamke mwenye ulemavu. Sio kwamba wanawake wenye ulemavu hawawezi la hasha watupe nafasi waone kama tutashindwa,” anasema na kuongeza kwamba wakati mwingine wanakosa nafasi kutokana na ukosefu wa taarifa.

Anasema ni vyema taarifa za fursa mbalimbali zikawa zinawafikia na pia jamii isiwaone kama hawawezi kutokana na ulemavu wao kwani kuna maeneo wanaweza kufanya vizuri kuliko hata watu waliokamilika viungo.

Anasema wakati mwingine walemavu wa viungo wanashindwa kutekeleza vyema majukumu yao kutokana na miundombinu katika maeneo yao ya kazi kutokuwa rafiki.

Ni kwa msingi huo anasisitiza umuhumu wa taasisi kuboresha miundombinu ili kuwarahisishia walemavu kufanya kazi kwa uhuru.

“Wakati mwingine mtu anataka kuomba kazi sehemu lakini anashindwa kutokana kukosekana kwa miundombinu rafiki, mfano baadhi ya mabenki, mahoteli na maofisi kadhaa,” anasema.

Anaongeza kwamba walemavu pia wanapenda kuonyeshwa upendo katika maeneo ya kazi na kupewa misaada kulingana na ulemavu pale inapohitajika.

Anasema ingawa Tanzania inapiga hatua katika kujenga majengo na kuzingatia mazingira ya watu wenye ulemavu tofauti na miaka ya nyuma lakini bado kuna maeneo wanasahauliwa na hivyo anamhimiza waziri mwenye dhamana kuweka msisitizo katika hilo.

Decarisa anatoa wito kwa mashirika binafsi na taasisi mbalimbali kuwakumbuka watu wenye ulemavu, hususani wanawake pale wanapokuwa katika harakati za kuajiri.

“Angalau kila shika lingeajiri mlemavu mmoja kwa sababu wapo wengi waliosoma na hawana kazi na pia naomba wasiwachoke watu wenye ulemavu wanapotuma maombi yao na ikiwezekana wapewe kipaumbele cha ajira ili kuweza kufikia dunia yenye usawa,” anasema.

Watu wenye ulemavu wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kunyimwa ajira au kukutana na miundombinu isiyo rafiki. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mtu mmoja miongoni mwa watu kumi katika jamii ni mwenye ulemavu.

Kwa hesabu hizo, Tanzania inakadiriwa kuwa na walemavu takribani milioni 3.4. Je, ni wangapi kati ya hao wamepewa ajira kulingana na sheria na sera tulizojiwekea kaka taifa?

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili.

Chanzo: www.habarileo.co.tz