Mtu mmoja amefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika maandamano ya wananchi wakiwemo wavuvi wa eneo la Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani hapa, wakituhumu askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), kuua wavuvi wenzao.
Tukio hilo lililotokea jana Mei 22, 2023 limeelezwa kuwa chanzo chake ni mgogoro wa mpaka baina ya wavuvi na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara iliyopo eneo hilo la Mto wa Mbu.
Akielezea tukio hilo, Diwani wa Kata ya Mto wa Mbu, Hussein Munga amesema kulikuwa na mgogoro wa mpaka baina ya wavuvi wa Kijiji cha Jangwani na hifadhi hiyo ambapo uliingiliwa kati na Mkuu wa wilaya hiyo kwa ajili ya utatuzi.
Amesema baada ya kufanyika kwa vikao viwili katika eneo hilo na wavuvi hao walichokuwa wanahitaji ni mpaka baina yao na eneo la hifadhi.
Amesema kuwa wiki iliyopita mpaka uliwekwa baada ya wataalam kutoka halmashauri hiyo kwenda katika eneo hilo, ila wavuvi hao hawakuridhika na kudai mpaka umesogea kwao zaidi.
"Ila leo asubuhi wavuvi watatu walijeruhiwa kule ziwani na askari wa Tanapa na baada ya wavuvi hao kujeruhiwa wenzao na wakafanya maandamano wakawa wanaelekea kwenye ofisi za Ziwa Manyara,"
"Ila wakati wanaelekea kule askari polisi wakawa wanajaribu kuzuia yale maandamano kwa kushirikiana na askari wa Tanapa na kwenye zile na kwenye purukushani inadaiwa mtu mmoja aliuwawa kwa kupigwa risasi na wengine kujeruhiwa,
"Bado tunaendelea kufuatilia kwani hata asubuhi wavuvi wanadai kuna wenzao wawili hawawaoni wanahofia nao wameuawa," amesema Diwani huyo.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Joshua Nassari amesema katika tukio hilo mtu mmoja amefariki na wengine saba wamejeruhiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela akizungumza kwa simu na Mwananchi, amesema kuwa yuko nje ya mkoa na alikuwa njiani kuelekea eneo hilo la tukio na kuwa atatoa taarifa baada ya kufuatilia.