Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mmoja afariki, mwingine ajeruhiwa na simba Ngorongoro

Simba Wazurura Mitaani Nairobi, Wananchi Watakiwa Kuwa Waangalifu Mmoja afariki, mwingine ajeruhiwa na simba Ngorongoro

Thu, 6 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Mtu mmoja Mkazi wa Kijiji cha Malambo, wilayani Ngorongoro mkoani hapa, Sironga Mepukori, amefariki dunia kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata alipokuwa akijaribu kupambana na simba aliyevamia shule.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu leo Alhamisi Juni 6, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Kanali Wilson Sakulo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Amesema tukio hilo lilitokea jana Juni 5,2024 mchana, ambapo simba huyo alivamia eneo la Shule ya Msingi Malambo, iliyopo Kata ya Malambo, wilayani Ngorongoro Mkoa wa Arusha.

"Ni kweli simba aliingia katika eneo la shule hiyo na wanafunzi walipomuona walitoa taarifa kwa uongozi wa shule ambao waliomba msaada kwa wananchi waishio jirani na shule hiyo ambao walijitokeza kwenda kusaidia,"amesema.

Mkuu huyo ameeleza kuwa miongoni mwa wananchi waliojitokeza ni ndugu wawili ambapo aliyefariki anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 23.

Sironga anadaiwa kufariki dunia wakati akipelekwa hospitali kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata wakati akipambana na simba huyo.

Ameeleza kuwa ndugu wa marehemu, aliwahishwa hospitali kwa ajili ya matibabu kutokana na majeraha aliyopata wakati wakipambana na simba huyo, pia mnyama huyo aliuawa na wananchi waliokuwa wamejitokeza shuleni hapo.

"Malambo kule ni karibu na pori Tengefu hivyo wanyama wakali wapo. Nitoe wito kwa wananchi wachukue tahadhari na pindi wanapoona wanyama wakali, watoe taarifa kwa wataalamu wa wanyamapori, badala ya kuchukua hatua wenyewe," ameongeza.

Chanzo: Mwananchi