Raia mmoja aliyetambulika kwa jina la Nassib Abdallah amefariki dunia huku askari polisi wawili wakijeruhiwa na magari kadhaa ya polisi kuharibiwa kufuatia ghasia zilizozuka wakati polisi wakijaribu kudhibiti vitendo vya ramli chonganishi vilivyokuwa vinafanywa na watu wanaojiita waganga katika vijiji vya Sunuka, Sigunga, Ilagala na Lubengera huko wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma ACP Filemon Makungu, amesema tukio hilo limetokea Juni 17 huko Ilagala wilayani Uvinza ambapo wananchi waliojichukulia sheria mkononi walifanya vurugu ikiwemo kufunga barabara kwa magogo, mawe, kuchoma magurudumu na kuharibu mali katika barabara ya Simbo-Kalya na kurusha mawe kwa askari polisi.
Awali iliripotiwa kuwepo kwa waganga matapeli maarufu kama 'Lamba Lamba' wakiwalaghai wananchi kuwa wana uwezo wa kufichua wachawi katika vijiji hivyo huku wakiwakusanya watu waliowadhania kuwa ni wachawi na kuwanyoa nywele, kuwachanja chale mwilini na kuwapaka dawa kwa lengo la kuwaondoa ushirikina huku wakitozwa fedha kiasi cha Shilingi elfu 30 na kuendelea.
Kufuatia hali hiyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, alifanya vikao vya uelimishaji kwa viongozi wa serikali za mitaa, viongozi wa dini, wazee na wananchi katika kata za Ilagala na Sigunga kuwaeleza madhara ya vitendo hivyo katika jamii na kupiga marufuku visiendelee lakini baadhi ya wanachi walikataa kutii marufuku hiyo na kuanzisha vurugu hizo na kujikuta kati mzozo na askari polisi.
Hata hivyo kulinagana na Kamanda ACP Makungu, jeshi la polisi limefanikiwa kurejesha hali ya amani katika wilaya ya Uvinza huku watu watano wanaotuhumiwa kushiriki vurugu hizo wakitiwa mbaroni na wengine wakiendelea kusakwa ili sheria ichukue mkondo wake.