Mtu mmoja amefariki dunia baada ya gari ndogo aina ya Toyota Hilux kugonga treni katika makutano ya reli na barabara eneo la Kilimahewa Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Mei 23, 2022, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu amesema ajali hiyo imetokea usiku wa kumkia leo na kusababisha kifo cha dereva wa gari hiyo, Michael Mgombela (34).
Mgombela ambaye ni mwanachama chama wa waendesha baiskeli Mkoa wa Morogoro alifariki dunia papo hapo baada ya kutokea ajali hiyo.
Kamanda Musilimu amesema Mgombela akiwa anaendesha gari hiyo alishindwa kuchukua tafadhari wakati akivuka njia ya treni na kusababisha ajali hiyo.
"Dereva wa gari ndogo amepoteza maisha baada ya kuvamia kiberenge katika makutano ya njia ya reli Kilimahewa Manispaa ya Morogoro"amesema Kamanda Musilimu.
Advertisement Kamanda Musilimu ametoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto, mikokoteni na watembea kwa miguu kuendelea kuchukua tafadhari wanapovuta katika njia za treni ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kwa watu kupoteza maisha na mali.
Mwenyekiti wa chama wa waendesha baiekeli Mkoa wa Morogoro (Uluguru bike), Goodwill Mkunda amesema kuwa kifo Mgombela maarufu Mwarafu Fighter ni pigo kubwa kwa chama hicho.
"Tumepata pigo kwa mwanachama wetu kufariki dunia na kama chama tutakaa pamoja kuona tunashirikiana na familia kwa karibu katika msiba huu." amesema Mwenyekiti Mkunda.