Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mlinzi adaiwa kumuua Nzota kwa risasi

RISASI 2222222222 Mlinzi adaiwa kumuua Nzota kwa risasi

Tue, 3 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tukio la mauaji ya kikatili lililoacha mashaka, limezua taharuki katika Kijiji cha Mlangoni kilichoko Kata ya Gararagua, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro baada ya mlinzi wa Watawa wa Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu kudaiwa kumpiga risasi na kumuua papo hapo mkazi wa kijiji hicho, Nicholas Nzota maarufu baba Sharon.

Nzota, ambaye ni Mkazi wa Kitongoji cha Kilari, alikwenda karibu na Shamba kuchungia mifugo la Watawa hao (Holly Spirit Sisters) linalomilikiwa na Kanisa Katoliki, Jimbo la Moshi akihoji sababu za walinzi waliokuwa karibu na Hospitali ya Charlotte, kuwashikilia wanawake wawili katika mazingira yenye utata baada ya kusikika wakipiga yowe kuomba msaada.

Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk. Christopher Timbuka, amesema tukio hilo la mauaji limetokea Oktoba mosi mwaka huu, majira ya saa 1:00 usiku karibu na hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa Dk. Timbuka, walinzi wa shirika hilo la Watawa walikuwa wamewashikilia mateka wanawake wawili waliowakuta eneo la mpakani mwa hospitali hiyo jambo ambalo lilileta vurugu baina ya wananchi na walinzi hao.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Yahaya Bwanamdogo, alisema tayari wanamshikilia mlinzi huyo kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mlangoni, Ezekiel Mloli, alisema ni kweli alipokea taarifa kwamba kuna mtu amepigwa risasi mpakani mwa shamba la Watawa hao na shamba linalomilikiwa na chama cha msingi, na alipofika eneo la tukio aliukuta mwili wa Nzota, ukiwa chini.

"Baada ya kuuona nilitoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi Sanya Juu na walikuja na kuuchukua mwili wa marehemu kuupekeka Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto kwa ajili ya kuuhifadhi.

"Unajua marehemu (Nzota) alifika katika eneo hilo baada ya kusikia sauti za kina mama wakiomba msaada.

Mlinzi huyo hii ni mara ya pili kupiga watu risasi miezi minne iliyopita alimpiga kijana mwingine risasi ya mguu na kuuvunja. Ameona haitoshi amerudia tena na kuua Mwananchi mwingine kwa risasi. tunaomba sheria ichukue mkondo wake maana tumechoka."

Mei mwaka huu, katika eneo hilo hilo, karibu na Shamba la Watawa wa Shirika la Kazi ya Roho Makatibu, wananchi wanadai mlinzi huyo huyo, alimpiga risasi ya moto mguuni, Boke Mollel, Mkazi wa Magadini akimtuhumu kutaka kumnyang'anya silaha, wakati wa ukamataji wa mifugo yake ikiwamo ng'ombe alioelezwa waliingia ndani ya shamba hilo.

Kutokana na matumizi hayo ya nguvu, hasa matumizi ya bunduki, wakazi wa Kitongoji cha Kilari, akiwamo Beatrice Shoo, wameiomba serikali na vyombo kuingilia kati sakata hilo kwa kuwa hata silaha iliyotumika Mei kujeruhi hawajui imerejeaje mikononi mwa mlinzi huyo.

Katika mkutano wa dharura ulioitishwa leo kijijini humo, Mbunge wa Siha na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amewasihi wananchi wa Kijiji cha Mlangoni na hasa Kitongoji cha Kilari kuwa watulivu wakati jambo hilo linashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

"Nawaombeni utulivu na uvumilivu mliounyesha toka jana, lililotokea tatizo hili muendelee kuhudumisha najua ni vigumu.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live