Serengeti. Binti wa miaka 19, Nyangi Nyahochaki mkazi wa kijiji cha Robanda wilayani hapa, ambaye ni mlemavu wa ubongo na viungo amekutwa na ujauzito wa miezi tisa.
Kitendo cha binti huyo kupata ujauzito kimeshangaza kwa kuwa haongei, hatembei, zaidi ya kucheka na ni mtu wa kukaa ndani tu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Nyerere, Tanu Warioba alisema walimpokea binti huyo Julai 19 akitokea Zahanati ya Robanda na baada ya kumpima walibaini ana ujauzito wa wiki 25 (sawa na miezi sita) na anatakiwa kujifungua Novemba mwaka huu.
“Hatuwezi kumhudumia lazima apelekwe kwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Musoma ili akatumie utaalamu atamzamlishaje, maana hawezi kulala chali wala kukaa, yeye ni ubavu tu ikizingatiwa ili utoe mtoto lazima ulale chali.
“Mbali na ulemavu unaomfanya ashindwe kujikunjua ana tatizo la mtindio wa ubongo (celebralpalsy), hili ni tatizo la mfumo wa fahamu linahusisha ubongo na neva za fahamu, unaathiri sehemu ya ubongo inayohusika na misuli, akifika kwa bingwa atajua namna ya kumsaidia kuanzia hatua ya sasa hadi kujifungua,” alisema.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Emiliana Donald alisema taratibu zikikamilika atapelekwa Musoma kwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake.
Pia Soma
- Wahofia kuondolewa kwenye maeneo ya kufanyia biashara
- Uhamiaji Tanzania yashikilia paspoti saba za mwandishi wa habari
- Rais John Magufuli kuzindua Terminal 3 muda mfupi ujao
- Serikali ya Tanzania yasaini mkataba ujenzi barabara ya lami Tanga - Pangani
Ujauzito wa binti huyo, ni kitendaliwi kwa Jumapili anayedai kuwa alipata wasiwasi baada ya kuona mabadiliko ya mwili wa mtoto wake wakati akimfanyia usafi (kumuogesha), ndipo alipoamua kumpeleka hospitali.
Akiwa wodi ya wazazi Hospitali Teule ya Nyerere mkoani Mara, Jumapili alisema hajui hatma ya binti yake itakapotimia miezi tisa ya kujifungua kwani hawezi kulala chali, ni ubavu tu.
Alisema ili bintiye akae ni lazima akalishwe kwenye beseni huku akihoji kwa mazingira hayo, upasuaji utafanyikaje?
“Awali, sikutilia shaka kama angeweza kuwa na mimba, nikadhani ni kipindi cha kupevuka, lakini nilishtuka kuona mstari kwenye tumbo wakati namkogesha na kwa kuwa haongei ilinilazimu kushirikisha majirani wakaniambia nimpeleke kwenye vipimo.
“Nilipofika Zahanati ya Robanda walitupa rufaa kwenda Hospitali Teule ya Nyerere na ikabainika ana mimba ya miezi sita, niliishiwa nguvu! Maana nawaza nitawezaje kuwalea wote (mama na mtoto) kwa hali yangu hii, kweli aliyeamua kuyafanya haya ameniweza,” alisema huku akifuta machozi.
“Pamoja na unyonge wangu kwa miaka yote 19, nimehangaika na mwanangu wa pekee kumlisha, kumuosha na huduma nyingine. Sasa kapewa mimba sijui itakuwaje…namwachia Mungu,” alisema Jumapili ambaye hamjui mwanaume aliyempa ujauzito bintiye.
Jumapili ambaye alikuwa na watoto watatu, wawili walifariki, alisema kazi yake ni kuuza kuni ili apate chakula kwa ajili yake na bintiye mlemavu.
Alisema awali, kila alipomaliza kumhudumia bintiye alimfungia ndani kwa kufuli na kwenda katika shughuli zake, lakini majirani walichukizwa na kitendo hicho na kumtahadhirisha kuwa ikitokea moto itawawia vigumu kumuokoa, hivyo akawa anaacha mlango wazi.
“Tangu utoto wake, hawezi kutembea wala kuongea zaidi ya kucheka tu, huduma zote kuanzia kula na kila kitu namfanyia mimi. Sikutegemea angetokea mwanaume (wa kumpa ujauzito), bora ningeendelea kumfungia ndani haya yasingetokea,” alisema.
Alisema aliyempa ujauzito bintiye imebaki kuwa fumbo kwani hawezi kuongea na anaomba Serikali ya kijiji na watu mbalimbali wamsaidie kwa kuwa hana fedha.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Robanda, Mrobanda Japani alisema kutokana na hali ya Jumapili kiuchumi na tatizo lililomtokea, uongozi umekubaliana kumsaidia gharama za matibabu kuanzia sasa hadi hapo bintiye atakapojifungua.
“Mama huyo anaishi kwa kuuza kuni, maisha yake yanajulikana ni magumu. Amefikia hatua ya kukata tamaa kutokana na alivyohangaika na mtoto wake. Tukio hili limemchanganya zaidi, tumekubaliana kupitia mapato ya kijiji yanayotokana na uhifadhi tumsaidie kama tunavyosaidia wengine kwenye elimu,” alisema Dk Warioba.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Emiliana Donald alisema taratibu zikikamilika atapelekwa Musoma kwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake.