Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkuu wa wilaya amsimamisha kazi Mwenyekiti wa Kijiji wa CUF

13265 Mkuu+pic TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Chemba. Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mkoani Dodoma, Simon Odunga amemsimamisha kazi Mwenyekiti wa Kijiji cha Olbolot Kata ya Mrijo, Abdalah Ally Suti (CUF) kwa tuhuma za ubadhirifu na kutosoma mapato na matumizi ya wananchi kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita.

Odunga ametoa agizo hilo Jumanne Agosti 21, 2018  kwenye mkutano uliofanyika kijiji hapo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wa eneo hilo.

Mkuu huyo wa wilaya amesema Mwenyekiti huyo atasimama kufanya kazi hiyo hadi hapo watakapojiridhisha na uchunguzi wa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji hicho.

Amesema kuanzia sasa Mwenyekiti huyo na wajumbe wote wa serikali ya kijiji hicho wanapaswa kuachia madaraka hayo na kuwapisha viongozi wa vitongoji vinne wa kijiji hicho kuongoza kwa kushirikiana na mtendaji wa kijiji.

"Na hii iwe funzo kwa viongozi wote wa vijiji vya wilaya ya Chemba, someni taarifa ya mapato na matumizi ya wananchi kwa kila miezi mitatu kwani nitawachukulia hatua sababu wananchi wanalalamikia hilo," amesema Odunga.

Awali, mkazi wa eneo hilo, Abasi Bakari amesema Mwenyekiti huyo hajawasomea mapato na matumizi ya miradi mbalimbali ya kijiji hicho kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita.

Bakari amesema kuna baadhi ya mapato ikiwemo asilimia za ushuru wa mazao, shamba la kijiji, mapato ya gulio na sehemu ya kuhifadhi mazao hivyo hawafahamu hesabu za miradi hiyo.

"Tangu awe Mwenyekiti kwenye hii awamu yake ya tatu kwa takribani wiki 44 hajasoma kwa wananchi mapato na matumizi ya miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo wana kijiji kubaki hewani juu ya fedha zao," amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo Suti alikiri kutosoma mapato na matumizi ya kijiji hicho kwa muda huo kutokana na kutokuwa na mtendaji wa kijiji.

Suti amesema aliandaa taarifa na alitaka kufanya mkutano huo na kusoma taarifa hiyo ya mapato na matumizi kwa wananchi ila mtendaji wake wa kijiji akahamishwa.

Amesema Ofisa Mtendaji mwingine alipofika eneo hilo akaugua ghafla kwa muda mrefu hivyo akashindwa kuitisha mkutano wa kusoma taarifa ya mapato na matumizi kwa wananchi.

"Mwezi Januari 2018 wakati najindaa kusoma taarifa hiyo yakatokea mafuriko kwenye eneo hili ambapo mimi na mkuu wa wilaya tukashirikiana kuokoa watu na kuwahamishia kwenye kambi," amesema Suti.

Amesema sheria, kanuni na taratibu hazijafuatwa kwani mamlaka sahihi na husika iliyomuweka ndiyo ilipaswa kumtoa na atafikiria kama ni kukata rufaa au kutoa taarifa mamlaka ya juu ya chama chake ila anaheshimu tamko hilo la mkuu wa wilaya.

"Mimi ni Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Chemba na huu ni mwaka wa 14 naongoza kijiji hiki ningekuwa mbadhirifu nisingechaguliwa kwa awamu tatu kuanzia mwaka 2004/2009 kisha 2009/2014 na mwaka 2014/2019," alisema Suti.

Kijiji cha Olbolot kilichopo Kata ya Mrijo Wilayani Chemba Mkoani Dodoma, awali kilikuwa ni kijiji ndani ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.

Chanzo: mwananchi.co.tz