Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam imemsimamisha kazi Mkuu wa Shule ya Sekondari Makumbusho, Juma Mulindani kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili za kuwanyanyasa wanafunzi kingono.
Hatua hiyo imekuja siku nne tangu Mwananchi imeripoti tuhuma hizo zinazodaiwa kufanywa na mkuu huyo wa shule Agosti 18 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa juzi na Manispaa ya Kinondoni ilieleza uchunguzi wa awali ulikamilika wiki iliyopita na sasa wameingia katika hatua ya pili na tatu ya kuchunguza udhibiti ubora wa elimu kabla ya kueleza kilichobainika.
Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kinondoni, Mtundi Nyamhanga amesema kwa sasa wanaendelea kujiridhisha na taarifa walizozipata na watatoa taarifa rasmi mwishoni mwa wiki.
“Kama mtumishi amehusika na suala hili atapelekwa Tume ya Walimu na tunapofanya uchunguzi wetu tunamuweka mkuu wa shule pembeni, anapisha kituo tufanye uchunguzi wetu na kama tukimhitaji tunamuita na kazi kubwa itafanywa na wadhibiti ubora,” amesema Nyamhanga.
Amesema tangu wamepata taarifa hizo wiki iliyopita, wamekuwa wakilishughulikia kwa kufuata sheria za kiutumishi katika kulishughulikia.
“Bado tupo kwenye uchunguzi pale zinakwenda timu tatu tofauti kila moja ina kazi yake na Mkurugenzi wa Halmashauri tumewasiliana na tunafanya kazi bega kwa bega.
"Timu ya awali wameshakamilisha uchunguzi na taarifa yao wanaikabidhi leo Halmashauri na timu ya wadhibiti ubora itaanza kazi yao kesho mpaka Ijumaa watakuwa wamekamilisha," amesema Nyamhanga.
Alisema baada ya chunguzi hizo kukamilika watatoa taarifa. "Kwa sasa mpaka tujiridhishe kuhusu taarifa zilizopo na yale tuliyoyapata katika uchunguzi wa awali na tukibaini kasoro vyombo vya dola vipo na kiutaratibu huwa tunachukua hatua kwa watumishi wote wanaovunja maadili," amesema.
Mbali na uchunguzi unaofanywa na Halmashauri, sakata hilo pia linachunguzwa na Ustawi wa Jamii pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Kamati hizo zinachunguza malakamiko hayo baada ya wanafunzi na wazazi waliozungumza na Mwananchi kueleza baadhi ya wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo na mwingine kulazimika kuhamishwa kutokana na kufanyiwa vitendo hivyo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa siku kadhaa ulibaini wanafunzi hao wamekuwa wakiitwa katika ofisi ya mwalimu huyo na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kushikwa maungo yao, hali inayowafadhehesha wanafunzi hao.
Mwananchi ilipomtafuta mwalimu Mulindani jana kutaka kujua kuhusu kusimamishwa kwake, hakupatikana katika simu yake ya mkononi.