Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkuu wa shule aeleza walivyomtoa Anna Same bila taarifa za vifo

85027 Pic+mwanafunzi Mkuu wa shule aeleza walivyomtoa Anna Same bila taarifa za vifo

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Same. Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Theresia of Calcuta iliyopo wilayani Same, Padri Christopher Mboya amesema kwa wiki tatu alikuwa hapati usingizi wa uhakika, akiwaza kuzuia Anna Zambi kupata taarifa za vifo na jinsi walivyomtoa shuleni.

Anna alipoteza wazazi wake wote na wadogo zake watatu Oktoba 25, muda mfupi kabla ya kuanza mtihani wa kumaliza elimu ya sekondari na walimu hawakutaka akatishe mitihani hivyo wakaamua kudhibiti habari zisimfikie.

“Ni ukweli usiofichika kwamba kwa wiki tatu mfululizo nilikuwa sipati usingizi,” alisema Padri Mboya.

“Nilikuwa na wakati mgumu sana kama mkuu wa shule kuhakikisha Anna anafanya mitihani yake kwa amani na salama bila kufahamu taarifa za vifo vya ndugu zake.”

Hata hivyo, alisema wakati mwingine alikuwa akijiuliza baada ya kumaliza mitihani yake anaenda wapi na watamwelezaje taarifa za vifo vya familia yake.

“Tulipata mawazo mengi kutoka kwa wadau wa elimu na wadau. Wengine waliniambia nimueleze lakini nikaona hapana,” alisema Padri Mboya.

“Nilikuwa na mawasiliano na mmoja wa familia hiyo kuangalia namna gani ya kuondoka hapa baada ya kumaliza mitihani yake.

“Tulikubaliana ndugu (baba yake mdogo) huyo ndiye aje amchukue, lakini nikamweleza Anna mtu fulani unamjua akasema ndiyo. Nikamwambia basi anaenda kwenye harusi Dar atakupitia hapa muondoke wote, akasema sawa, ila nilimwambia huyo ndugu yake aje na keki siku hiyo.

“Ndugu huyo alikuja na keki basi Anna alifurahi pamoja na kusherehekea na wanafunzi wenzake na sisi walimu wake na baada ya hafla hiyo wakaanza safari ya kurejea nyumbani kwao. Hakika nina zaidi ya miaka 13 ya upadri na nimekuwa nikipambana na magumu, lakini hili lilikuwa gumu kwangu.

“Hii ni kwa sababu nilibeba tatizo hili kwa wiki tatu na hata siku Anna anaondoka hapa shuleni, nilisimama mahali nikiangalia ni kweli anaondoka getini bila kujua suala hili.

“Niliinua mikono juu na kumshukuru Mungu maana lilikuwa si jambo jepesi kwangu.”

Akizungumzia jinsi walivyodhibiti taarifa za vifo kumfikia Anna, padri huyo alisema kwanza aliitisha kikao cha uongozi wa shule kutafuta njia bora ya kumsaidia ili amalize mitihani yake salama.

“Niliitisha kikao cha wafanyakazi wote wa shule na nikawaeleza kwa msisitizo kwamba mfanyakazi yeyote atakayesababisha kuvuja kwa taarifa hizo atawajibika kwa namna yoyote ile,” alisema Padri Mboya.

Alisema alihakikisha mawasiliano yote nje na ndani ya shule yanafungwa.

Alisema walizuia wanafunzi kuangalia televisheni na kuzima inteneti za maktaba ili kuepusha uvujaji wa taarifa hizo ambazo zingeweza kumuweka katika wakati mgumu zaidi mwanafunzi huyo na kushindwa kutimiza ndoto zake.

“Tuliwaambia wanafunzi kuwa kwa muda uliobaki kabla hawajaanza mitihani, hawaruhusiwi kuangalia TV wala intaneti kwa sababu wanajiandaa na mitihani hiyo,” alisema.

“Lakini tuliimarisha ulinzi getini. Kulikuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingia ndani ya geti la shule na baadhi ya wanafunzi waliomaliza kipindi cha nyuma waliokuwa wanakuja kuchukua vyeti vyao tulilazimika kuvihamishia getini ili wasaini hapo hapo getini na kuondoka.”

Alisema uongozi wa Jimbo Katoliki Same pamoja na uongozi wa shule wamejipanga mwishoni mwa mwezi huu kwenda kumfariji mwanafunzi huyo na wataambatana na baadhi ya wazazi wa wanafunzi waliohitimu na Anna.

Akizungumzia tukio hilo, msaidizi wa mkuu wa taaluma, Amosi Mashini alisema Anna alikuwa akifanya vizuri kitaaluma tangu ajiunge na shule hiyo.

“Amekuwa ni mwanafunzi bora katika mitihani hapa shuleni,” alisema Mashini.

“Tangu aanze shule hajawahi kutoka kwenye kumi bora ya wanafunzi waliokuwa wakifanya vizuri katia mitihani yao.

“Ni miongoni mwa wanafunzi tunaotegemea kuwa watafaulu vizuri tena kwa daraja la kwanza.”

Chanzo: mwananchi.co.tz