Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkuu wa mkoa akunwa kasi ukusanyaji mapato Tunduru

42aefd327569cb45edd254044f966692 Mkuu wa mkoa akunwa kasi ukusanyaji mapato Tunduru

Thu, 14 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa kufanikisha kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 121.87 katika mwaka wa fedha 2019/2020 na kuifanya halmashauri hiyo kushika nafasi ya kwanza kimkoa.

Mkuu huyo wa mkoa amesema hayo juzi wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika mjini Songea, ambapo alieleza kuwa halmashauri hiyo imeonesha mfano bora katika ukusanyaji mapato na kuzitaka halmashauri nyingine kuongeza jitihada ili kufikia malengo waliyopewa.

Alisema mafanikio hayo yametokana na dhamira ya kweli ya watumishi wa halmashauri hiyo kudhibiti upotevu wa fedha zinazokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali na kudhibiti matumizi ya ovyo ambayo yanasababisha baadhi ya halmashauri kushindwa kufikia malengo yake.

Aidha, Mndeme aliipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwani tangu imeanza kutumia Stendi Kuu ya Shule ya Tanga kuanzia Januari Mosi mwaka huu imeongeza ukusanyaji mapato ya ndani yatokanayo na ushuru wa stendi na choo kutoka Sh 200,000 hadi Sh 900,000 kwa siku.

Pia alieleza kufurahishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) ambayo kwa mwaka wa fedha 2019 imeweza kukusanya Sh 15,885,857,987 sawa na asilimia 94 na katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2020 ilikusanya jumla ya Sh 16,365,091,735.82 ambazo ni sawa na asilimia 105.

Mndeme alisema kutokana na kazi nzuri zinazofanywa na idara, sekta na taasisi za serikali mkoa huo unatarajia kuongeza mapato yatokanayo na kodi pamoja na ushuru kwa kuwa barabara ya Ushoroba wa Mtwara imefunguka na kutoa fursa nyingi za kibiashara ambazo zipo katika maeneo mengine ya nchi na nchi jirani za Malawi na Msumbuji.

Akizungumzia hali ya chakula katika msimu wa mavuno 2019/ 2020, alisema mkoa ulifanikiwa kuvuna tani 1,355,509 za mazao ya chakula wakati mahitaji ya wakazi wa mkoa huo ni tani 469,172 na kubaki ziada ya tani 886,337.

Alisema uzalishaji huo unaufanya mkoa wa Ruvuma kuendelea kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa mara ya pili mfululizo na hayo ni matokeo ya wananchi wa mkoa huo kuendelea kujituma katika shughuli za kilimo.

Chanzo: habarileo.co.tz