Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurungezi Ubongo aingilia kati migogoro

F824817e47d7d5b1c22d1b40e2146847 Mkurungezi Ubungo aingilia kati migogoro

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKURUGENZI wa Manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic ameingilia kati mgogoro uliopo baina ya Mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam, Allasta Mlay na jirani yake Johanes Sangawe, kwa kuamuru hatua stahiki zichukuliwe ili haki itendeke.

Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa, unamhusu mlalamikaji Mlay na jirani yake huyo ambaye ni mlalamikiwa Sangawe kwa kutiririsha maji machafu ya chooni kwenye nyumba yake hali ambayo imesababisha nyufa katika nyumba yake na kuhatarisha magonjwa ya mlipuko.

Gazeti hili lilitaka kujua maagizo yaliyotolewa na Mkurugenzi huyo wa Manispaa Dominic kwa mlalamikiwa huyo kama yametekelezwa, alieleza kuwa aliyafikisha kwa wasaidizi wake ambao alitegemea watakuwa wameyasimamia, na kuagiza mlalamikaji huyo afike tena ofisini kwake kama bado changamoto hiyo inaendelea.

“Kama bado tatizo hilo linaendelea aje ili jirani yake apelekwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

Akizungumza na Habari Leo mlalamikaji huyo Mlay alieleza changamoto hiyo aliyoipata kwa zaidi ya miaka 10 lakini bado haijatatuliwa pamoja na kutoa taarifa maeneo mbalimbali bila mafanikio.

Kwa mujibu wa Mlay, mwaka 2018 aliyekuwa Bwana Afya katika kata hiyo, Kawa Kafuru alifanikiwa kupeleka maji hayo kwenye vipimo na kubaini kuwa ni ya kinyesi lakini hakuna jitihada zozote zilizochukuliwa na mhusika wala wenye mamlaka.

Alisema, mwaka 2016 aliandika barua yake ya malalamiko kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Upendo uliopo Kata ya Saranga Kimara iliyohusu utiririshaji maji machafu na maji ya mvua katika fensi ya nyumba yake bila mafanikio.

Pia alisema mwaka huu aliandika barua nyingine kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo kuhusu changamoto yake hiyo ambayo bado haijapatiwa ufumbuzi pamoja na kutolewa kwa maelekezo kuwa changamoto hiyo itatuliwe.

“Afya yangu na familia yangu ipo hatarini sana na ikumbukwe maji yale yana acidi nyumba yangu imeharibiwa vibaya sana na maji hayo machafu hivyo inaweza kutitia au kuvunjika wakati wowote. Pia ikumbukwe kuna milipuko ya magonjwa,” ilisema sehemu ya barua hiyo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo.

Pia aliandika barua kwa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) kuhusu changamoto hiyo anayoipata bila mafanikio yoyote.

Kwa upande wake aliyekuwa Bwana Afya katika Manispaa hiyo ya Ubungo ambaye kwa sasa amehamishiwa NEMC, Kawa Kafuru alisema kuwa malalamiko hayo aliyakuta mezani hivyo aliposoma taarifa za upimwaji wa maji yale ilionyesha kuwa maji yale yalikuwa na uchafuzi wa kibinadamu.

“Katika suala hilo sheria inataka nini?ilitaka apeleke mahakama ya Sokoine shtaka likasomwa mlalamikaji akaweka wakili baadaye kesi ikafutwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mlalamikiwa Sangawe alisema kuwa kuna baadhi ya maagizo waliyopewa tayari wameshayafanyia kazi ila mengine walikuwa wanasubiri kumaliza mahakamani tayari wamemaliza hivyo wanarudi kutekeleza.

“Suala limeenda kote na maamuzi yaliyotolewa ndiyo tumeyatekeleza. Kulikarabati shimo tumelirekebisha,”alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz