Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amefikisha ombi kwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI la kutenguliwa uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Sekiete Yahya kwa madai ya kukiuka maelekezo ya Kamati ya Usalama Wilaya ya Septemba 28 mwaka jana kuhusu uuzwaji wa viwanja.
Kamati hiyo ilizuia uuzwaji wa viwanja Na. 194 na 195 vilivyopo kwenye Mtaa wa Rwegasore katikati ya jiji hilo, lakini wao waliamua kuviuza kwa Sh. milioni 500 kila kimoja.
Malima amesema kuwa ofisi yake imeandika barua hiyo kwa Ofisi ya Rais - TAMISEMl kutokana na mkurugenzi huyo kuonyesha alichokiita utovu wa nidhamu mara kwa mara kwa viongozi wenzake na kuomba hatua zichukuliwe kwa madai kuwa hafai kuendelea kuwa katika mkoa huo.
"Tumemkuta Mkurugenzi wa Jiji na makosa makubwa ya kukiuka maelekezo ya Kamati ya Usalama Wilaya na ameonyesha kutokuheshimu mamlaka zilizo juu yake kwa utovu huo wa nidhamu alioufanya ambapo alitengeneza hoja ya kuuza viwanja hivyo isivyo halali na tumebaini kuwa endapo vingeuzwa kwa njia ya mnada vingeuzwa kwa zaidi ya Sh. milioni 500 kila kimoja," alisema Malima alipozungumza na waandishi wa habari jana.
Alikumbusha kuwa Septemba 28 mwaka jana, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya iliitaka Halmashauri ya Jiji isiviuze viwanja hivyo bila ya idhini ya kamati hiyo lakini wao wakaamua kuviuza kwa Sh. bilioni moja kwa kisingizio kuwa wamepata rukhsa ya kuuza viwanja hivyo kutoka Ikulu," Malima amesema.
Katika hatua nyingine, Malima ametangaza kuwasimamisha kazi kwa siku saba kupisha uchunguzi watumishi wanne wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza huku akitoa ombi kwa Ofisi ya Rais Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji hilo kutokana na madai ya utovu wa nidhamu.
Waliosimamishwa kazi kuanzia leo ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Ardhi, Robert Phales, Ayubu Kasuka Halima Nassor na Yuster Zephrine.
Amesema ofisi yake imeunda kamati ya kuchunguza sakata hilo kwa siku saba itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Maadili wa Kanda ya Ziwa, Godson Kweka huku ikihusisha wataalamu kutoka Ofisi za TAKUKURU, Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Amefafanua kuwa awali Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa viwanja hivyo vimeuzwa kinyemela bila kumtaarifu Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na halmashauri imekiri kuviuza na kusema wamefanya hivyo kwa rukhsa ya Ofisi ya Rais Ikulu, TAMISEMl na Wizara ya Ardhi jambo ambalo si kweli.
"Viwanja hivi haviruhusiwi kuuzwa, kufanyiwa ujenzi wala kuendelezwa kwa namna yoyote mpaka pale suala hili litapomalizika na endapo itaonekana wamiliki wanastahili kuendelea, watapata taarifa na kwa upande wa halmashauri ninaagiza fedha zilizopatikana kwenye uuzwaji wa viwanja hivyo zisitumike ili itapobainika kumekuwa na ukiukwaji wa uuzwaji, basi wamiliki watarejeshewa fedha zao," Malima amesema.
Vilevile, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilitoa onyo kali kwa Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo, watumishi wa Idara ya Fedha na Uhasibu, Ofisa Ununuzi, Mwanasheria na Mkaguzi wa Ndani ikiwataka kujitathmini kwenye utendaji wao kwa kuwa wameonekana kutosaidia halmashauri ipasavyo na itatoa onyo kali kupitia Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa.
"Mwanza haiwezi kuwa kichwa cha mwendawazimu kwamba kila mmoja anakuja kupiga fedha, kama watu wameingia kufanya tamaa na kuhusika na suala hili, basi kwa dhamira yetu kama viongozi wa mkoa tutakwenda kutoa mfano kwenye suala hili kwa kutoa adhabu kali," ameonya Malima.