Mkuu mpya wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba,amesema kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri atakayeshindwa kujibu hoja za ukaguzi hatakwenda likizo.
Serukamba alisema hayo jana wakati akizungumza na watendaji kutoka wilaya zote za mkoa huu wakiwamo wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa mkuu wa mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato alisema kwamba atakachokiangalia ni mapato halisi na sio asilimia zilizokusanywa.
"Tusipimane kwa 'percentage' tuangalie kiasi cha mapato kilichokusanywa maana kuna mchezo wa halmashauri kuweka makadirio kidogo ya ukusanyaji wa mapato na baadaye kuonekana makusanyo yaliyopatikana ni mengi," alisema.
Serukamba alisema atakaa na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi,Wenyeviti wa halmashauri pamoja na madiwani kuangalia makadirio ya mapato yanayowekwa katika kila halmashauri na namna ya kuyaongeza kila mwaka.
Kuhusu bima ya afya, alisema atahakikisha kila mwananchi anakuwa na kadi ya bima ya afya ya CHF au NHIF ili waweze kupata huduma za matibabu bila usumbufu.
Serukamba alisisitiza suala la usafi wa mazingira kwa kila mji linapewa kipaumbele pamoja watumishi wanakuwa wanadhifu wanapokwenda kazini.
"Usafi hauhitaji bajeti ya serikali ni utaratibu tu, haiwezekani unakuja ofisini ukiwa umevaa malapa lazima tuhakikishe miji yetu inakuwa misafi," alisema.
Kuhusu kilimo alisema suala hili ataliwekea mkazo kwa kuhakikisha watu wanalima kweli na kujiwekea malengo kila mwaka ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Mambo mengine atakayoyashughulikia ni migogoro ya ardhi,anuani za makazi na suala la amani usalama katika mkoa.
Naye Mkuu wa Mkoa aliyemaliza muda wake Dk. Mahenge, aliwashukru watumishi wote wa Mkoa wa Singida kwa ushirikiano waliompa katika kipindi alichokuwa mkoani hapa na kutaka ushirikiano huu wauonyeshe kwa RC Serukamba.
Dk.Mahenge alisema mtaji mkubwa wa maendeleo ni amani na usalama na kwamba anashukru ameuacha mkoa ukiwa na amani