Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi ashindwa kulipa bil 2, arudishwa rumande

Mkurugenzi Jatu Mkurugenzi Jatu

Tue, 3 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JATU Public Ltd, Peter Gasaya (32), anayetuhumiwa kujipatia Sh. bilioni 5.1 kwa udanganyifu, ameelezwa na mahakama kuwa ili awe nje kwa dhamana anatakiwa awasilishe mahakamani Sh. bilioni 2.6.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JATU PLC, Peter Gasaya, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa masharti ya dhamana. Hata hivyo mshtakiwa huyo ameshindwa kutimiza masharti hayo na hivyo kurudishwa rumande.

Gasaya anatuhumiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka SACCOS ya JATU kwa madai kuwa ataizalishia faida huku akijua si kweli.

Sharti hilo la dhamana lilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio wa mahakama hiyo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa masharti ya dhamana.

Hakimu Mrio alimweleza mshtakiwa kuwa anaweza pia kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Pia mshtakiwa huyo atatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho na vitambulisho ambavyo kila mmoja atatia saini bondi ya kiasi hicho cha fedha.

Baada ya mshtakiwa kusomewa masharti hayo, alishindwa kuyatimiza na alirudishwa rumande hadi Januari 11, mwaka huu, kesi yake itakapotajwa tena.

Awali akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru, alidai kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2022, mshtakiwa akiwa ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo, alijipatia Sh. 5,139,865,733 (Sh. bilioni 5.14) kwa njia ya udanganyifu kutoka JATU SACCOS.

Mshtakiwa anadaiwa kuchukua fedha hizo kwa madai kuwa atazipanda fedha hizo na kuzalisha faida huku akijua si kweli.

Baada ya mshtakiwa kusomewa shtaka lake, alikana kuhusika na tuhuma hizo, Hakimu Mrio akisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana inayozidi Sh. milioni 300.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live