Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amemshukia mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Zefrin Lubuva na kutaka mamlaka yake kutomlipa mshahara wa mwezi Februari, 2020 hadi atakapobadilika.
Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari 14, 2020 baada ya mkurugenzi huyo kushindwa kujibu swali alilomuuliza katika kikao maalumu cha kamati ya ushauri ya Mkoa huo kuhusu
halmashauri hiyo kushindwa kutoa asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
"Mkurugenzi naomba kupata taarifa ya makusanyo yenu na kiasi mlichotoa kwa vikundi vya kina mama, vijana na watu wenye ulemavu, mmetoa kwa asilimia ngapi na kwa nini hamjafikia malengo kama Serikali ilivyoelekeza, “ amesema Mghwira.
Baada ya swali hilo, mkurugenzi alipewa kipaza sauti ili kujibu lakini alitaka ajibu mtaalamu mwingine jambo ambalo Mghwira alilipinga na kutaka ajibu mwenyewe.
Licha ya kutakiwa kujibu Lubuva alishindwa na kunyamaza kimya na kumfanya mkuu huyo wa Mkoa kumtaka mwenyekiti wa halmashauri hiyo kujibu.
Pia Soma
- Mwenyekiti Halmashauri, madiwani wawili waikimbia Chadema, Mbunge afurahia
- Serikali yadhibiti ngono Siku ya Wapendanao
- Makonda akwepa kuzungumzia kupigwa ‘stop’ kuingia Marekani
Baada ya maelezo hayo, Mghwira alimtaka tena Lubuva kusimama na kutoa majibu kwa nini hawajafikia lengo la kutoa asilimia 10 kama Serikali inavyoelekeza lakini kwa mara ya pili alishindwa kujibu.
"Mkuu naomba radhi tugange yajayo" amesema Lubuva na kisha kuketi.
"Sasa wanaokulipa mshahara wasikulipe mwezi huu, tugange yajayo mpaka huo mwezi Machi,” amesema mkuu huyo wa Mkoa.
Mghwira amezitaka halmashauri za wilaya kuhakikisha zinatekeleza maelekezo ya Serikali ya kutoa asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vikundi vya kina mama, vijana na watu wenye ulemavu.
Halmashauri ya Mwanga hadi kufikia Januari, 2020 ilikuwa imetoa Sh17 milioni kwa vikundi vya wanawake na hakuna kikundi cha vijana wala walemavu kilichopewa fedha hizo.