Askari wa Jeshi la Polisi wa Kituo cha Mabatini, Kijitonyama wanadaiwa kumuua kwa kumpiga risasi Riziki Azan (29), mlinzi wa baa maarufu jijini Dar es Salaam ya Board Room, iliyopo Sinza Mori, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea saa saba usiku wa jana, wakati askari hao wakitaka kumkamata mmoja wa wahudumu katika baa hiyo, wakidai alikuwa anafanya biashara ya kujiuza.
Kutokana na tukio hilo la mauaji, Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia askari wake wawili kwa uchunguzi na hatua zaidi za kisheria zimeelezwa zitachukuliwa dhidi yao.
Akisimulia tukio hilo, Meneja wa baa hiyo, Frank Tukai alisema askari hao walifika kwenye baa hiyo saa sita usiku wakitaka kumkamata mmoja wa wahudumu aliyekuwa akitoka kwenye duka jirani na baa hiyo.
Alisema mhudumu huyo alikuwa ametoka kwenye sherehe ya mfanyakazi mwenzake, baada ya kunywa alinyanyuka na kwenda dukani, ndipo wakati akirejea, askari hao walimkamata wakimtuhumu kuwa anajiuza na kutaka kuondoka naye.
“Baada ya kuona hivyo niliwafuata na kuwaeleza huyu dada ni mfanyakazi wangu ametoka kwenye sherehe ya mwenzao, hapa wamekuja kuweka vyombo, hawakuelewa, ndipo malumbano yalipoanza,” alisema.
Alidai askari hao wawili wakiwa wanaonyesha wamekunywa, hawakutaka kuelewa maelezo ya meneja huyo, ndipo mmoja akiwa ameshika bunduki, mwingine alikwenda kwenye gari akiwa amevaa sare na kuchukua bunduki na kurudi alipokuwa mwenzake.
“Huyu mmoja aliendelea kumchoma choma yule dada na bunduki, lakini mimi nikawa namshauri anavyofanya si vizuri, isije ikafyatuka, lakini yeye alinijibu huyu anaongea sana tunahitaji kuwanyoosha,” alidai.
“Yule wa pili aliporudi alikuwa kashika bunduki mkono wa kulia, akanikunja na kunivuta, wakati tunajibizana, yule mwingine alikoki bunduki. Kabla sijageuka nikasikia imefyatuka, ikaenda kugonga kioo cha kabati nikaona mtu anadondoka chini,” alidai.
Alidai baada ya tukio hilo walianza kutishia watu kisha wakaondoka eneo hilo na kuwa haikuwa mara ya kwanza, kwani kuna siku amewahi kumtolea mkurugenzi bunduki.
Baada ya hapo, Tukai alidai polisi walimchukua yeye na kwenda naye Kituo cha Polisi Mabatini ambapo walimpiga na wakamweka ndani.
“Baada ya tukio lile mkurugenzi (wa baa) alimpigia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi ambaye alimuahidi kulifanyia kazi. Nikiwa pale walikuja askari wakauliza aliyefanya tukio, yeye na wenzake wakawekwa ndani,” alidai.
Mwananchi ilimtafuta Kamanda Kitinkwi ambaye alisema atafutwe Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kuwa yeye ndiye msemaji.
Jana jioni, taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Gabriel Pupa ilieleza kuwa Novemba 29, maeneo ya Sinza Mapambano askari wawili walimjeruhi kwa risasi mtu mmoja Razaki Azan (29) mlinzi binafsi wa baa ya Board Room, ambaye baadaye alipoteza maisha.
Alisema Jeshi la Polisi limeshawakamata askari hao na mambo ya kisheria yanakamilishwa kwa hatua za kisheria haraka kadiri iwezekanavyo. Kamanda Pupa alisema mwili wa Azan umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala kukamilisha uchunguzi.
Mkurugenzi wa baa huyo, Frank Temba alisema si mara ya kwanza kwa askari huyo kufanya tukio kama hilo, akisema kuna siku alikwenda kwenye baa hiyo saa tisa usiku akiwa na wenzake wawili wakiwa na gari ndogo wakimtaka meneja awape fedha za mafuta.
Alidai wakati mwingine huwa wanachangia mafuta gari za doria kama ni magari ya polisi na meneja alipomkatalia kwa kuwa fedha ni za ofisi na kuna magari mengine yameshapita, alianzisha mzozo.
“Nilipoenda alitukana matusi makubwa. Nilimwambia mimi ni mtumishi wa umma, lakini pia ni mmoja wa wamiliki, alinitukana na kwenda kwenye gari kuchukua bunduki na kunitishia na ndio huyohuyo aliyefanya tukio,” alidai Tesha, akizungumza kutoka Dodoma.
Kwa mujibu wa shuhuda aliyekuwepo eneo hilo ambaye hakuta jina lake liandikwe, aliungana na meneja kusema kuwa askari hao walifyatua risasi walipotaka kumkamata mhudumu wa baa hiyo wakidai anajiuza ilhali alikuwa anatoka kwenye sherehe ya mdogo wake.
Alisema msichana huyo ambaye pia walikuwa wote kwenye sherehe, walikuwa wamekaa wote (Board Room), aliwaacha na kwenda dukani na wakati anarudi aliona nguo inauzwa duka la jirani, wakati amekwenda, ndipo polisi walipomkamata wakimtuhumu anajiuza.
“Baada ya kumshikilia walimuita meneja, alipokwenda akawa anawaelewesha polisi kuwa huyo ni mfanyakazi wake, wao wakawa hawaelewi kukawa kama kuna mvutano baada ya polisi kutaka kuondoka naye,” alidai.
“Polisi aliyekuwa amevaa sare, akaenda kwenye gari na kuchukua bunduki, akarudi akawa anatishia watu, akawa anaenda huku akiwatisha watu, tukasikia risasi imepigwa tukaona mwanamume ameanguka chini,” alidai shuhuda huyo.
“Baada ya kuona vile, walimuacha pale aliyepigwa risasi wakamchukua meneja na kwenda naye kwenye gari kisha wakawasha gari na kuondoka na watu wakaanza kupiga kelele,” alidai.