Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi Dodoma atoa siri ya mapato lukuki

9692 DODOMA+PIC TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Siku moja baada ya Rais John Magufuli kulisifu Jiji la Dodoma kwamba limefanya vizuri katika makusanyo, Mkurugenzi wake Godwin Kunambi ameanika hadharani vyanzo vya mapato yake na kuwa ardhi ndiyo iliyowabeba.

Akizungumza leo Agosti 2 amesema  mafanikio hayo yamekuja baada ya kutangaza mauzo ya idadi kubwa ya viwanja kwa wakazi na watu wanaohamia makao makuu.

Hata hivyo Kunambi amesema kulikuwa na wizi mkubwa wa mapato ya ndani na kwamba vyanzo vingi vilikuwa havijulikani.

Alisema kuwa watendaji walikuwa wakikadiria kidogo ili wakusanye na kuvuka lengo ili wapongezwe.

Akiapisha viongozi mbalimbali aliowateua juzi Ikulu, Rais Magufuli aliwataka viongozi wengine akiwamo  Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Godwin Kunambi kutaja mikakati mikuu minne ambayo italiwezesha jiji la Dodoma kuanza kujitegemea ifikapo 2022/23 ili kuondokana na hali ya utegemezi wa ruzuku kutoka serikali kuu.

 

Mkurugenzi huyo amesema Halmashauri ya Jiji ilikuwa na makisio ya Sh 86,356,902,921 kwa mwaka 2017/18 lakini walikusanya jumla ya Sh 80,480,772,845 sawa na asilimia 93 ya malengo.

“Kwa makusanyo ya vyanzo vya ndani tulilenga kukusanya Sh20 bilioni lakini hadi mwisho tulikuwa tumekusanya Sh 25bilioni ambazo ni asilimia 120 ya malengo,” amesema Kunambi.

Hata hivyo Meya wa Jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe amesema huu ni wakati wa kufikiri zaidi kutafuta vyanzo vingine kwani suala la ardhi ni la muda na wakati wowote viwanja vinaweza kuisha.

Profesa Mwamfupe ameagiza wataalam kuzunguka kata zote 41 kutafuta vyanzo vya mapato vilivyokuwa vinafichwa na kutumia vizuri fedha wanazokusanya ili kujenga vitega uchumi.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz