Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkuranga watakiwa kuepuka majanga ya moto

16efc079abff9d4f108f1946e592ac2b Mkuranga watakiwa kuepuka majanga ya moto

Thu, 30 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIKA kukabiliana na majanga ya moto yanayosababishwa na shughuli za kiuchumi, kilimo na uchomaji mkaa pembezoni mwa barabara, wananchi wilayani Mkuranga, mkoa wa Pwani, wametakiwa kuachana na utamaduni huo ili kuepusha majanga hayo.

Akizungumza na wananchi kwenye mkutano uliofanyika katika kijiji cha Kisemvule juzi, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Mkuranga, Fransisko Chunji, alisema tabia hiyo inayoshika kasi ina madhara makubwa moto unapolipuka.

“Baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia ya kuchoma moto kama njia mojawapo ya kusafisha mashamba, huku wengine wakichoma mkaa pembezoni mwa barabara kuu ya kuelekea mikoa ya Kusini jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya watu.”

"Ajali zitokanazo na moto hujitokeza mara kwa mara na kwa magari yanayosimama kandokando mwa barabara baada ya kuharibika ni hatari endapo moto unawake kwani yanaweza kulipuka, hivyo ni vema watu wakaachana na utamaduni huo ambao siyo mzuri wa kusafisha mashamba kwa kuchoma moto na wanaochoma mkaa wafanye shughuli hizo mbali na barabara," alisema.

Kamanda Chunji alisema tahadhari hiyo ya moto pia inatakiwa kuchukuliwa na wamiliki wa vibanda vya mama na baba lishe vilivyo kando mwa barabara na kuwaagiza viongozi wa vitongoji, vijiji na kata kusimamia maelekezo hayo kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa kwa watakaokiuka.

“Jambo hili linapaswa kusimamiwa na viongozi ambao wako karibu na wananchi kwa kuwapatia elimu ya madhara ya moto kwa wanaofanya shughuli zao kando mwa barabara kwani ni hatari hasa kwa magari yanayotumia mafuta ya petroli," alisema.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara wa mitungi ya gesi wafike ofisini kwake ili wapatiwe maelekezo ya kina yanayolenga tahadhari kwa ujumla dhidi ya wananchi ili kuepuka majanga yanayoweza kujitokeza endapo moto utatokea.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisemvule, Omari Makunge, alisema atatumia vikao vya vitongoji na kijiji kufikisha elimu hiyo, huku akiiomba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuiangalia kwa jicho la huruma wilaya hiyo ambayo haina gari la zimamoto kwani kwa sasa wanategemea kutoka wilayani Temeke.

Chanzo: habarileo.co.tz