Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurabita umewafungulia wakulima Mufindi fursa za kukopa

57aec91ccc5266548bc3152d262d87b0 Mkurabita umewafungulia wakulima Mufindi fursa za kukopa

Tue, 2 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

“WANANCHI waliopata hati za hakimiliki za kimila baada ya urasimishaji wa mashamba yao ya chai walipatiwa mafunzo yaliyowezeshwa na Mkurabita (Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania) kuhusu matumizi ya hati hizo kiuchumi na kuunganishwa na taasisi za fedha zikiwamo benki.”

“Mafunzo hayo yalizihusisha pia taasisi mbalimbali ambazo ni wadau zikiwamo Bodi ya Chai Tanzania, Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (TASHTDA), Benki ya CRDB na wataalamu wa kilimo, maendeleo ya jamii na ushirika kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.”

Ndivyo inavyoeleza Taarifa ya Urasimishaji Ardhi na Kujenga Uwezo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji, Netho Ndilito na kusomwa na Ofisa Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Jeswald Ubisimbali, mbele ya Kamati ya Uongozi (Bodi) ya Mkurabita iliyokuwa wilayani Mufindi, Januari 25, 2021.

Kamati hiyo ilikuwa katika ziara ya ufuatiliaji wa urasimishaji wa ardhi na biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ya Iringa, Mbeya na Njombe.

Ikiwa wilayani Mufindi katika Mkoa wa Iringa, kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Daniel Ole Njoolay, ilitoa hatimiliki za kimila kwa wananchi wa Kijiji cha Lugodalutali kilicho katika Kata ya Igombavanu, Tarafa ya Sadani.

Kijiji cha Lugodaluteli kina wakazi takriban 1,500 wanaojishughulisha na kilimo, ufugaji na ujasiriamali.

Katika hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa hati za hatimiliki za kimila 342 kati ya 800 zilizoandaliwa kijijini hapo, taarifa iliyosomwa na Anderson Chogo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Lugodalutali, Sailas Kiwuyo, inasema: “Kupitia urasimishaji mashamba, tumepata elimu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji na sasa tuna idadi kubwa ya vyanzo vinavyotunzwa na jamii inatambua umuhimu wa kutunza mazingira.”

Kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, mwaka 2011/2012, Mkurabita ulijenga uwezo katika halmashauri hiyo kwa kutoa mafunzo ya nadharia na vitendo katika vijiji 24 vinavyolima chai.

“Mashamba 2,270 katika vijiji 24 yalipimwa na hatimiliki za kimila 2,205 zikaandaliwa kutokana na uwezeshaji uliofanywa na Mkurabita kwa kushirikiana na Bodi ya Chai Tanzania na TASHTDA,” anasema Ubisimbali.

Mufindi ni moja ya halmashauri zilizopewa kipaumbele mwaka 2011/2012 mkoani Iringa kwa kujengewa uwezo na Ofisi ya Rais-Ikulu, kupitia Mkurabita kwa ajili ya urasimishaji wa ardhi vijiji na kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia rasilimali wanazomiliki.

Halmashauri hii ina vijiji 121. Kati ya hivyo, vijiji 113 vimepimwa mipaka yake na 52 vimeandaliwa mipango ya matumizi bora ya ardhi hadi sasa.

Hadi kufikia mwaka 2012 wakati wa utambulisho wa Mkurabita, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ilikuwa imeandaa na kusajili hati za hakimiliki za kimila 57 katika vijiji vitatu vya Kilolo, Kasanga na Itimbo.

“Mkurabita imewezesha mradi wa urasimishaji wa mashamba ya chai katika vijiji 24 wilayani Mufindi. Mashamba 2,289 yamepimwa na hati 2,283 zimeandaliwa na kukabidhiwa…” inasema taarifa.

Vijiji 24 vilivyonufaika na upimaji na utoaji wa hati za hakimiliki za kimila katika mashamba ya chai wilayani Mufindi ni Ikaning’ombe, Nandala, Igoda, Ifupira, Itona, Kidete, Ikwega, Mkalala, Mninga, Ihomasa, Kasanga na Udumuka.

Vingine ni Lwang’a, Kilolo, Kibao, Lufuna, Sawala, Mpanga, Mtwango, Ihefu, Ludilo, Ifwagi, Mkonge na Luhunga.

Mintarafu manufaa ya utekelezaji wa shughuli za kujenga uwezo na manufaa ya hatimiliki za kimila, taarifa hiyo inasema ni pamoja na wakulima 144 na viongozi 20 wa vyama vya ushirika vya wakulima kupatiwa mafunzo ya kilimo bora cha chai, utunzaji wa kumbukmbu za shughuli za kilimo cha chai, fursa mbalimbali katika kilimo cha chai na upatikanaji wa mikopo kwa mkulima mmoja mmoja na kupitia ushirika wa zao la chai kutoka taasisi za fedha.

Baada ya uwezeshaji, taarifa inasema wakulima 54 walitumia hati hizo za kimila kopa Sh 429,840,000 katika taasisi za fedha wilayani Mufindi zikiwamo benki kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Imebainika kuwa, Benki ya CRDB imewakopesha wakopaji watatu kwa kutumia hati hizo. Mikopo hiyo ina thamani ya Sh 225,000,000. Benki ya MUCOBA imetoa mkopo wa Sh 141,000,000 kwa wakopaji saba, Benki ya NMB ikitoa Sh 30,000,000 kwa mkopaji mmoja na Tujikomboe SACCOSS imetoa mikopo ya Sh 33,840,000 kwa wakopaji 43.

Meneja wa Biashara wa Benki ya CRDB-Mufindi, Gasper Mlola, na Mwakilishi wa Benki ya TPB, Japhet Peter, wanasisitiza kuwa, hatimiliki za kimila zinatambuliwa na kutumika na benki zao kama dhamana kwa waombaji wa mikopo hivyo, wenye hati hizo wajitokeze katika benki zao kupata mikopo.

Nico Fox, mkulima wa chai katika Kijiji cha Mtwango wilayani Mufindi, anatoa ushuhuda kwamba alitumia hatimiliki ya kimila kupata mkopo wa Sh milioni 150 kutoka Benki ya CRDB baada ya kurasismisha shamba lake, hali iliyomwezesha kuboresha uzalishaji na kutanua wigo wa kupata mapato.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake waliopokea hati, Hassan Lugenge, alisema: “Tunashukuru Mkurabita na Rais John Magufuli maana sisi tumepata hati hizi bure, wengine wanalipia pesa nyingi…”

Taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi inasema: “Wananchi wetu wamenufaika na urasimishaji ardhi kwa namna mbalimbali ikiwamo umiliki wa pamoja wa ardhi katika familia unaowawezesha wanawake kumiliki na kutumia ardhi na uwepo wa usalama wa miliki za ardhi hizo baada ya kurasimisha na kupata hati.”

Inaongeza: “Tunaushukuru Mkurabita kwa uwezeshaji ilioufanya katika halmashauri yetu kwa ajili ya urasimishaji ardhi vijijini na kwa kutujengea uwezo na kutupatia vifaa muhimu vya urasimishaji hali iliyoiwezesha halmashauri kwa kiasi kikubwa kuendelea na urasimishaji.”

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Festo Mgina anasema: “Mufindi tumenufaika sana na mchakato wa urasimishaji kwa uwezesho wa Mkurabita na hii ni kwa kuwa tuliupokea na kuufurahia ndiyo maana mpaka sasa tunazidi kufurahia matunda ya Mkurabita.”

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William, anasema jamii sasa haipaswi kukwepa upangaji wa matumizi bora ya ardhi, upimaji na urasimishaji mashamba kwa kuwa ni kichocheo cha amani na maendeleo ya kiuchumi.

Anasema kupitia urasimishaji, vyanzo 1700 vya vimetambuliwa wilayani Mufindi na kuwekewa kinga ili vitumike kwa manufaa ya taifa.

Mratibu wa Mkurabita, Dk Seraphia Mgembe, anasema halmashauri zote zikitambua umuhimu wa urasimishaji biashara na ardhi, Watanzania watafika mbali kimaendeleo kwa kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya urasimishaji na kupungua kwa umaskini.

“Tafiti zinaonesha kuwa, penye urasimishaji, kiwango cha umaskini ni kidogo, na pasipo na urasimishaji hali ya umaskini ipo juu,” anasema Dk Mgembe.

Anaongeza: “Watu wasiogope mikopo benki, bali waone ni ufahari kwa ajili ya kufufua na kukuza mitaji yao na kujiletea maendeleo na bahati nzuri, benki sasa zinatambua na kupokea hatimiliki za kimila kama dhamana kwa mkopo na wenyewe wamethibitisha hapa.”

Akielezea faida za urasimishaji ardhi, Dk Mgembe anasema ni pamoja na kuondoa migogoro baina ya mtu na mtu, mtu na kijiji, kijiji na kijiji, wakulima na wafugaji na hupunguza dhuluma kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia hasa wanawake wakiwamo wajane.

“Ukiwa na hatimiliki mtu anakuwa na uhakika na imani ya kuingia ubia na wewe katika biashara na miradi mbalimbali na pia, unaweza kuitumia kwa dhamana katika vyombo vya sheria kama mahakama,” anasema Dk Mgembe.

Mbele ya wananchi hao wenye furaha kijijini hapo, Ole Njoolay anasema: “Hati hizi si za kufungia sandukuni au kwenye kabati, zitumieni kwa kukopa mitaji katika taasisi za fedha na kuzingatia nidhamu ya kurejesha mkopo ili wengine wakope na wewe ukope zaidi.”

Chanzo: habarileo.co.tz