Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurabita: Hatimiliki za kimila huepusha ukatili wa kijinsia

E1f8b3cbf77490ba58eab559b1c0d77b Mkurabita: Hatimiliki za kimila huepusha ukatili wa kijinsia

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

HATI za hakimiliki za kimila zinazotolewa baada ya kurasimisha ardhi na makazi zimetajwa kama moja ya silaha kubwa kupambana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kiuchumi unaowaathiri zaidi wanawake hasa wajane.

Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), Dk Seraphia Mgembe na Ofisa Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Geofrey Mwaijobele, walisema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumzia faida za urasimishaji ardhi na mashamba na kupata hati za hakimiliki za kimila.

Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mkurabita, Daniel Ole Njoolay, ametaja faida nyingine za kurasimisha ardhi na kupata hati za hakimiliki za kimila kuwa ni pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi baina ya mtu na mtu, mtu na kijiji, kijiji na kijiji na baina ya wakulima na wafugaji.

Kwa nyakati tofauti wilayani Mufindi katika Mkoa waIringa, Mbarali mkoani Mbeya na Njombe, Ole Njoolay alisema hatimiliki za kimila zinatumika hata kwa mikopo katika benki ili kukuzia mitaji na kutoa usalama na uhakika wa miliki ya ardhi.

Mjini Njombe, Dk Mgembe alisema wakati Kamati ya Uongozi ya Mkurabita ilipofika ofisini kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe kuwa, miongoni mwa faida za kurasimisha ardhi na kupata hatimiliki za kimila, ni pamoja na kuruhusu umiliki wa pamoja wa kisheria wa ardhi baina ya mke na mume katika familia na kutoa haki sawa kwa wote.

“Urasimishaji huchochea usawa wa kijinsia dhidi ya tamaduni za ukatili na unyanyasaji wa kijinsia hasa kiuchumi unaotoa mwanya kwa wanawake kudhulumiwa hasa wajane ambao huathirika zaidi wanapofiwa na waume zao na ndugu kutaka kuwanyang’anya ardhi, mashamba na makazi,” alisema Dk Mgembe.

Akaongeza: “Hati za hakimiliki za kimila hufanya watu kuishi kwa haki na usawa katika umiliki hata kama mmoja amekufa na pia, hati hizi hutumika hata kwa dhamana katika vyombo vya sheria na kuongeza imani kwa watu kuingia ubia na wewe katika miradi na uwekezaji mbalimbali.”

Hivi karibuni katika uwekaji wa jiwe la msingi katika Masjala ya Ardhi ya Kijiji cha Kapyo wilayani Mbarali iliyojengwa na Mkurabita, Mwaijobele alisema kwa kurasimisha ardhi na kupata hatimiliki ya kimila, si rahisi kwa mume au mke kunyang’anywa ardhi kwa kuwa hutambua umiliki wa wanafamilia hao kwa majina na picha zao.

Akiwa ofisini kwake alipotembelewa na kamati hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Katarina Revocati, alisema urasimishaji ardhi mkoani Njombe ni jambo muhimu kwa kuwa kuna ardhi nzuri na madini mbalimbali yakiwamo makaa ya mawe na madini ya chuma.

“Watu wanakuja sana huku kwa kuwa hali ya hewa na ardhi ni nzuri kwa mazao mbalimbali na madini ndiyo maana hata asilimia 70 ya mazao yanayozalishwa hapa, ni ziada inayouzwa na kulisha watu wa mikoa mingine…” alisema Katarina.

Chanzo: habarileo.co.tz