Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkondo wa maji chini ya ardhi waibua hofu Moshi

Mkondo Wa Maji Mkondo wa maji chini ya ardhi waibua hofu Moshi

Sun, 2 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Maji yanayotoka chini ya ardhi katika makazi ya wananchi na baadhi ya maeneo ya biashara eneo la Ngangamfumuni, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, yameibua hofu ya usalama.

Kwa mara ya kwanza maji yaliibuka mwaka 2020 na kuathiri shughuli za ujenzi wa mradi wa kimkakati wa mkoa huo wa stendi ya kimataifa ya mabasi ya Ngangamfumuni na makazi ya wananchi yaliyo pembezoni mwa mradi huo.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, hayati Anna Mghwira aliagiza wataalamu wa miamba kupiga kambi eneo hilo.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya kuanza utekelezaji wa mradi huo ambao ulizalimika kusimama. Ulitengewa zaidi ya Sh17 bilioni kwa ajili ya utekelezaji.

Mwaka 2023 kwenye kikao cha baraza la madiwani alipohojiwa kuhusu ucheleweshwaji wa mradi huo, Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa ya Moshi, Richard Sanga alisema ulianza mwaka 2019 na ulisimama kuanzia mwaka 2020 baada ya kukumbwa na misukosuko mingi iliyosababisha kushindwa kukamilika mwaka 2021.

"Mradi huu ulianza mwaka 2019 na ulikuwa na bajeti ya Sh28 bilioni, Serikali ilitoa Sh7 bilioni ambazo zilionekana haziwezi kumaliza mradi, ikafikia uamuzi wa kupunguza ukubwa wa mradi kwa tukatoa jengo moja la mradi wa hoteli, tukabakia na mradi mmoja wa stendi ambao utagharimu Sh17 bilioni," alisema wakati huo.

Hali kwa sasa

Katika tukio lililoibuka Mei 25, katika eneo hilo maji yamezingira zaidi ya nyumba 10, huku pia yakivunja barabara ya lami yakitafuta pakutokea.

Visima vitatu vilivyochimbwa katika mradi kupunguza maji hayo vimejaa na kuyamwaga kwenye mitaro maalumu iliyotengenezwa eneo hilo.

Diwani wa eneo hilo ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Moshi, Stuart Nkinda amesema bado hawajafanya tathmini kujua ni kaya ngapi zimeathirika.

Mkurugenzi wa Bonde la Pangani, Segule Segule aliyewahi kushiriki katika utafiti wa maji hayo, amesema mwanzoni kulipoibuka changamoto hiyo walifanya tathmini ya kina na wataalamu wengine kutoka Dar es Salaam na kubaini kilichotokea eneo hilo ni kutokana na aina ya miamba iliyopo.

"Maji yalipotokea tulifanya tathmini ya kina sisi Bonde la Pangani na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na wataalamu wengine. Tulibaini ni matukio ya kiasilia ambayo maji yanajitokeza mahali kama ambavyo chemchem inajitokeza katika maeneo mengine kutokana na mpangilio na uimara wa miamba iliyopo eneo husika na udongo," amesema.

Maji yanayotoka chini ya ardhi yakiwa yamevunja barabara ya lami eneo la Ngangamfumuni Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph.

Amesema kilichotokea katika eneo la Ngangamfumuni ni kutokana na kuchimbwa, akieleza kwa baadhi ya maeneo kama maji yalikuwa karibu lakini yamezuiwa na miamba, yanaweza kutoka na kuleta athari.

"Ngangamfumuni maji yanatoka mpaka usawa wa juu, kuna kitu kwenye sayansi ya maji tunaita ‘water table’ ni usawa wa maji katika eneo husika chini ya uso wa ardhi, usawa huo sasa wakati mwingine huwa unapanda kutokana na kiwango cha maji kinachohifadhiwa katika eneo husika, eneo lile linaonekana ndiyo hifadhi kuu ya maji upande wa juu," amesema.

"Kwa hiyo tunaangalia namna bora ya kuendana nalo lakini siyo jambo ambalo linaweza kupata suluhisho kirahisi. Ni kwamba maji yale yanalegeza ardhi na athari ni kwamba yanaathiri misingi ya nyumba na kuleta madhara kwenye nyumba za watu,” amesema

Amesema takwimu zilizochukuliwa awali zilionyesha maji yalikuwa yamepanda kwa mita nne, lakini kwa sasa yamepanda tena kidogo kwa mita kama tatu.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye amesema wakati tatizo hilo lilipojitokeza mwaka 2020 wataalamu wa UDSM walifanya utafiti katika eneo hilo na kubaini uwepo wa mikondo mitatu ya maji katika eneo hilo.

Amesema baada ya mikondo hiyo kujaa maji, hutafuta miamba ambayo ni dhaifu na hivyo kuruhusu kupita.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa Bonde la Pangani na wizara husika, watakaa kuangalia ni namna gani ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.

"Ni kweli kuna sintofahamu kidogo japo siyo kubwa ya maji kutafuta njia ya kutoka na kusababisha athari ndogondogo kwa baadhi ya nyumba na sehemu za biashara kutokana na maji kutoka chini ya ardhi," amesema.

"Kutokana na tafiti zilizofanywa miaka minne iliyopita na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na wataalamu wengine walionyesha kwenye eneo hilo la Ngangamfumuni kuna mikondo mitatu ya maji, mkondo mmoja ni mkubwa na mingine miwili ni midogo, na inaenda kukutana huko mbele," amesema.

Alisema baada ya utafiti kufanyika, wataalamu walitoboa visima vya maji vitatu vikubwa katika eneo la mradi wa stendi ya mabasi na kwamba, hivi sasa vinapandisha maji vyenyewe na kumwaga kwenye mitaro.

"Kama Serikali tunaangalia ni jinsi gani tunaweza kutafuta na kufuata mikondo hiyo kuangalia ni sehemu gani ya kutoboa ili kutengenezwa mahali maji yanapoweza kutokea juu kupunguza ukubwa wa tatizo," amesema.

Wasemavyo wananchi

Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesema maji hayo yanawapa usumbufu mkubwa, kutokana na kujaa hadi kwenye makaro ya vyoo.

Eva Temba, mmoja wa wananchi waliopo katika eneo hilo na mfanyabiashara wa nyumba ya kulala wageni, amesema maji yalianza kuonekana siku kadhaa zilizopita na kwamba kadri zinavyozidi kwenda maji yanaongezeka na kuwa kero kubwa.

Amesema hali hiyo inamuathiri kwani hata wateja wanashtushwa na wingi wa maji yaliyopo.

“Watu wanaogopa kuingia na hata kwenye mauzo tunapata shida, kwa sababu watu wana wasiwasi," amesema.

Naye Evod Tairo, mkazi wa eneo hilo amesema maji ni mengi hivyo wanapata shida ya kuyaondoa kila wakati.

"Miaka minne iliyopita tulikumbwa na hili tatizo maji yalikuwa ni mengi na mali ziliharibika ndani. Maduka nayo yaliathiriwa, sasa hii hali imejirudia tena,” amesema.

Amesema wataalamu wa miamba walitoa suluhisho lakini hali imejirudia, hivyo ameiomba Serikali iangalie cha kufanya wasiathirike zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti