Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkindi: Kilimo bado hakijapewa hadhi ya kuwa uti wa mgongo

58266 PIC+MKINDI.png

Mon, 20 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Japo kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania, sekta hiyo inachangia asilimia 30 tu ya pato la Taifa.

Asilimia 80 ya wakulima wa Tanzania wanaishi vijijini wengi wakiwa wanawake. Sekta hiyo inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo magonjwa, ukosefu wa zana bora za kilimo, upungufu wa wataalamu, ukosefu wa masoko ya mazao na migogoro ya ardhi.

Akijadili changamoto hizo katika majadiliano na Mwananchi, mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Maua Tanzania (Taha) ambaye pia ni mwenyekiti mpya wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Jacquiline Mkindi anasema bado sekta ya kilimo haijapewa kipaumbele.

Mkindi anashauri mbinu za kufanya ili kuboresha nchini.

Swali: Kwa sasa unasimamia taasisi hii inayohusu sekta ya kilimo, unadhani kwa nini kilimo kinachoajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania kimeshindwa kutoa mchango mkubwa katika uchumi kitaifa?

Majibu: Kwanza kabisa (kilimo) ni kipaumbele, lakini bado hakijapewa ile hadhi ya kuwa ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu. Watu wengi wanaofanya kilimo bado wanafanya kwa mazoea, ni asilimia chache sana ya watu wanaofanya kilimo cha kisasa.

Pia Soma

Wakulima pia wanapata changamoto kama vile ukosefu mitaji, upatikanaji wa masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi, tozo nyingi kwenye viuatilifu, ukosefu wa sera zinazowalinda wakulima.

Swali: Tanzania ifanye nini ili kilimo kiwe na pato kubwa, kwa maana ya uzalisha kuwa mkubwa na wenye tija, kama vile kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya mbolea na masoko?

Majibu: Kwanza ni kufanya kilimo kuwa biashara, kuwekeza kwenye ngazi zote kuanzia wataalamu wa kilimo ili kuweza kufanya kilimo cha kisasa na si cha mazoea, kuweka kumbukumbu ya mapato na matumizi, kuongeza thamani mazao ya horticulture (kilimo cha matunda, maua na mbogamboga) ili kujipatia kipato zaidi. Serikali inapaswa kuweka mwavuli wa kulinda maslahi ya wakulima kuanzia kwenye pembejeo hadi wakati wa kuuza kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.

Swali: Licha ya Tanzania kuwa na eneo kubwa linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, bado umwagiliaji upo chini. Unaiishauri nini Serikali kwa masilahi ya Taifa?

Majibu: Serikali inatakiwa kuwawezesha wananchi wafaidike na maeneo haswa ya umwagiliaji. Tumeona mara kadhaa wakulima wanavyoharibiwa mazao yao kutokana na kulima kwenye maeneo yenye vyanzo vya maji.

Ni sawa lakini wakulima wakipewa muongozo na Serikali wa maeneo yapi wafanye kilimo na kiasi gani ili watunze mazingira itasaidia kilimo hiki kuliingizia taifa kipato zaidi.

Swali: Ukiwa mkurugenzi mtendaji wa chama cha wazalishaji wa mboga na maua unaona sekta hiyo imekuwa kiasi gani? Kuna changamoto gani na mnakabiliana nazo vipi?

Jibu: Sekta imekuwa kwa kiasi kikubwa na tunaishukuru Serikali hadi sasa horticulture ina kitengo maalum ndani ya wizara ya kilimo.

Sekta pia inachangia pato la wananchi lakini na taifa kwa ujumla, sekta pia imeajiri vijana kwenye minyororo yake yote ya thamani.

Changamoto kubwa ni wakulima wengi hawajawezeshwa kufanya kilimo na tozo na kodi bado zinawaelemea licha ya juhudi kubwa inayofanywa na Serikali kuna maeneo bado yamebanwa.

Changamoto nyingine sugu ni upatikanaji wa masoko ya ndani na ya nje, mkulima anaweza kuzalisha kwa ubora lakini akakosa soko, mambo haya yamekuwa yakirudisha nyuma wakulima na kupelekea kukata tamaa ya kufanya kilimo kabisa.

Swali: Mnawasaidiaje wakulima wadogo, hasa wanawake na vijana waliowekeza kwenye kilimo cha mbogamboga na matunda ili kufaidika kiuchumi hasa katika masoko ya ndani na nje ya nchi?

Jibu: Asilimia kubwa ya wakulima wetu wanaangukia kwenye hili kundi la wanawake na vijana na tunashukuru wengi wao wanafanya vizuri na tayari kuna ambao wameshafanya vizuri na kweli tunajivunia wao.

Tumekuwa tukiwashirikisha kwenye fursa za masoko ya ndani na nje, kuna ambao wana mikataba mizuri na wanauza mazao yao nje ya nchi. Wapo waliofaidika na hiyo kwetu sisi ni fahari.

Swali: Suala la masoko nalo limekuwa kero kubwa, unadhani Serikali ifanye nini?

Jibu: Masoko ni changamoto kama nilivyosema awali, masoko yako ya ndani na ya nje na yote yanaweza kuwasaidia wakulima kama wakipata fursa hizo.

Kikubwa Serikali inachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wakulima wanakuwa na mazingira wezeshi ya kufanya shughuli zao za kilimo. Pia iwape nafasi wakulima kuuza mazao nje ya nchi bila ya kuwa na vikwazo vingi, kuruhusu wataalamu kutoka nje kuja kuwaongezea ujuzi wakulima wetu ili waweze kuendana na matakwa ya masoko ya dunia.

Swali: Suala la mabadiliko ya tabia nchi limeanza kuleta athari kwa wakulima, je ACT imejipangaje kuwasaidia wakulima katika hilo?

Jibu: Mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakileta madhara kwa wakulima wengi na sisi ACT tungependa kuwaomba wakulima kuacha kutegemea kilimo cha mvua, badala yake wafanye kilimo cha umwagiliaji kinachoweza kufanyika kwa mwaka mzima bila shida.

Pia watunze mazingira kwa kuhakikisha wanatunza vyazo vya maji na kuhakikisha shughuli zao haziharibu mazingira.

Swali: Katika masoko, zao la korosho limekuwa gumzo kubwa katika msimu wa 2018/19, unadhani nini kifanyike kwa misimu ijayo?

Jibu: Korosho imeleta shida kutokana na kukosa soko la kuaminika, wakulima wamelima lakini hawana sehemu ya kuuzia.

Kwa msimu ujao ni vyema wakulima wakajipanga kujua ni wapi kuna soko hasa la korosho na baada ya hapo kulima kulingana na matakwa ya soko.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inapaswa kuona fursa za masoko ya korosho yako wapi na kuhakikisha msimu ujao wa zao hili wakulima wanafaidika.

Swali: Ili kuleta tija katika kilimo, suala la viwanda nalo linahitajika, je Tanzania tuko wapi na kwa nini usindikaji mazao bado ni changamoto?

Jibu: Viwanda hasa kwa mazao bado ni changamoto ndio maana bado wakulima wengi wanalia na masoko. Tanzania hatupo sehemu mbaya ila kuna jambo la kufanyika ili hali iwe nzuri zaidi.

Tunahitaji viwanda vya kuongezea thamani mazao ya wakulima wetu ili waweze kusindika na kuyatumia kwa matumizi mbalimbali.

Hatupo pabaya ila kuna sababu ya kupigia debe suala la kuwa na viwanda kwani hili litasaidia wakulima wetu kuwa na uhakika wa masoko ya mazao yao lakini fedha nyingi pia zitabaki nchini kwani kutakuwa hakuna ulazima wa kusafirisha maparachichi halafu baadaye uagize bidhaa zilizotengenezwa na parachichi kutoka nje ya nchi.

Hiyo itasaidia sana wakulima kuendelea na kuona matunda ya kilimo.

Fahamu zaidi

Jacqueline Mkindi ni mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wazalishaji wa mboga, maua na matunda (Taha) na Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT).

Anayo shahada ya kwanza ya heshima ya sayansi katika misitu utunzaji wa viumbe wa asili na shahada ya uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA) ni mtaalamu wa maendeleo aliyejikita katika biashara.

Ametoa mchango mkubwa katika uongozi akileta mabadiliko yaliyoingiza mamilioni ya dola katika sekta ya mboga, matunda na maua nchini na amewezesha kujenga uhusiano wa kimkakati kati ya Serikali, sekta binafsi na na wadau wa maendeleo.

Mchango wake wa kibiashara uliowezesha michakato wa kitaifa na kimataifa umewezesha kuikuza Taha.

Chanzo: mwananchi.co.tz