Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkenda: Rombo msipuuze chanjo ya virusi vya corona

B1456948cf039fe90b1a30bba626712c.jpeg Mkenda: Rombo msipuuze chanjo ya virusi vya corona

Wed, 8 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MBUNGE wa Rombo, mkoani Kilimanjaro, Profesa Adolf Mkenda, amewataka wananchi wa jimbo hilo waiamini serikali na wasipuuze chanjo ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa covid -19.

Alitoa rai hiyo jana wakati wa ufunguzi wa mradi wa matundu 16 ya vyoo vya wanafunzi na walimu katika Shule ya Msingi Mbomai Juu, Kijiji cha Mbomai, Kata ya Tarakea Motamburu, wilayani Rombo.

Alisema janga la covid-19 limeathiri wananchi wa Rombo na kusababisha vifo lakini baadhi ya watu wamekuwa wakipuuza kwenda kupata chanjo.

“Covid-19 ipo na imeua sana Rombo na sababu ni kutokana na wilaya hii kuwa na mwingiliano mkubwa wa watu, kila siku magari zaidi ya 10 yanaondoka kwenda mikoani, watu wetu pia ni wajasiriamali wanakuja na kutoka hivyo maambukizi hapa ni mengi mno, chanjo ni hiari ila naomba mchanje,” aliwahimiza wananchi hao.

Aliwaeleza wananchi hao kuwa wakichanja wataokoa maisha yao na ya wengine na kwamba yeye, familia yake na viongozi wengine wameshachanja.

“Inasikitisha kuona idadi ya waliochanja Rombo ni ndogo sana, ndugu zangu mchanje, wazungu hawawezi kutuua ili waje kuchukua nini, viamba? Dawa nyingi zinatoka kwao pia chanjo za watoto wanatoa hadi bure, sisi tulichanja chanjo ya pepopunda leo mnaogopa chanjo ya covid- 19, chanjeni hasa wale wenye umri wa miaka zaidi ya 50,” alisema Profesa Mkenda.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kanali Hamisi Maigwa, alisema zaidi ya wananchi 2,000 wamechanja wilayani humo na mwitikio ni mdogo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz