Ni takribani miaka miwili imepita sasa tangu Michael Buchayanda ashambuliwe na kuachwa na ulemavu wa kudumu.
Buchayandi (32), mwenyekiti wa Kitongoji cha Rondo, Kata ya Mchukwi wilayani Kibiti ni miongoni mwa viongozi wa vijiji walioshambuliwa na watu wasiojulikana wakati wa mauaji yaliyotokea katika baadhi ya wilaya za mkoa wa Pwani mwaka 2017.
Kwa Selina Mponye (30), mke wa Buchayanda, tukio la mauaji hayo bado lipo kichwani mwake na linazunguka kama mkanda wa video.
Ilikuwa ni takribani siku 14 tangu Selina ambaye ni mke wa Buchayandi atoke kujifungua mtoto wake wa nne ndipo alipokutana na tukio hilo lililobadilisha historia ya maisha ya familia yao.
“Nakumbuka siku hiyo tulimaliza kula chakula cha usiku na sote tukaingia ndani kulala, kabla hatujapitiwa na usingizi mida ya saa tano tukasikia mlango ukivunjwa,
“Waliingia watu kadhaa na kutuamuru tutoke nje, walimkamata mume wangu, na kumshambulia kwa kumpiga na rungu kisha kutoka naye nje, kumbe huko walikuwepo wengine wakaondoka naye. Kwa muda huo sikuelewa wamekwenda wapi,” anasema.
Wale wengine waliosalia wakaendelea kuwaamrisha Selina na wanafamilia wengine kutoka nje ya nyumba bila kufahamu walitakiwa kwenda wapi.
“Niliwaomba waniruhusu angalau nimvalishe nguo mtoto wangu mchanga kwa sababu ya baridi, walikataa na kusisitiza nitoke naye nje.
“Tulipotoka tuliwashuhudia wakiichoma nyumba yetu kwa kutumia mafuta yaliyokuwa kwenye pikipiki ya mume wangu, iliyokuwa imeegeshwa nyumbani. Wakaenda kwenye kibanda cha nje tulichokuwa tunahifadhia vyakula na tulikuwa tumetoka kuvuna mpunga, mihogo na mahindi vyote vikachomwa,” anasema.
Wakati yote hayo yakiendelea hakuna aliyekuwa akitambua ni wapi Buchayandi alipelekwa, lakini baada ya muda ukasikika mlio wa risasi kutoka porini.
Mlio huo uliwashtua wote wakiwamo wale waliokuwa wanawapa amri, wakapeana ishara na kuanza kujificha kwenye migomba iliyokuwapo eneo hilo na hatimaye wakaondoka wakiwa wamewaacha Selina na wenzake uwanjani wakiendelea kushuhudia nyumba ikiteketea.
Baada ya utulivu kutawala kwa muda wakanyanyuka na kutafuta namna ya kujiokoa na kuanza kukimbilia kwa majirani ndipo walipobaini kuwa uvamizi huo haukufanyika kwao pekee. “Kumbe wale watu walijigawa kwa makundi walivamia pia nyumbani kwa mtendaji na mwenyekiti wa kijiji wakafanya uharibifu kama uliofanyika kwetu.
“Hapo bado hatukujua mume wangu yuko wapi, ikabidi kazi ya kumtafuta ianze ndipo alipokutwa yeye na wenzake wakiwa wametupwa porini kwenye dimbwi la damu.”
Anasema huo ndio ukawa mwanzo wa kunusuru maisha ya Buchayandi kwani alipelekwa hospitali na kupatiwa matibabu ya awali kabla ya kuhamishiwa Muhimbili alikokaa kwa wiki tatu. Shambulio alilolipata Buchayandi liliharibu macho yake na kumsababishia upofu.
Familia ikapata pigo kubwa kwanza masaibu yaliyomfika Buchayandi aliyekuwa tegemeo, pili kukosa makazi baada ya nyumba yao kuchomwa moto. Swali likawa baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali Buchayandi na familia yake wanakwenda kuishi wapi?
Jibu lilikosekana ndipo Selina alipoamua kuwapeleka watoto kwa ndugu zake na yeye kuzunguka na mumewe wakitafuta msaada.
“Tulipata fedha kidogo tukaenda kupanga Kinondoni ili iwe rahisi kutafuta msaada wa matibabu ya macho kwa mwenzangu maana bado alikuwa akilalamikia maumivu makali,” anasema.