Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkasa wa mlemavu wa uziwi kupoteza mtoto hospitali

Mlemavuupiiic Data Mkasa wa mlemavu wa uziwi kupoteza mtoto hospitali

Sun, 2 Oct 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Sasa ni dhahiri kuwa vituo vya afya na hospitali zinalazimika kuwa na wataalamu wa lugha ya alama, watakaowezesha mawasiliano kati ya wagonjwa wenye ulemavu wa kutosikia na wataalamu wa afya.

Kisa cha mjamzito Subira Upurute, mkazi wa mkoani Mtwara, kinasikitisha na kupiga kengele ya haja ya kuwapo kwa wataalamu wa lugha ya alama.

Kisa chake kiko hivi kama anavyosimulia mwenyewe:

"Nikiwa mjamzito nilikuwa nikienda kliniki mara kwa mara mambo mengi yanazungumzwa,  lakini siyapati kutokana na kikwazo cha mawasiliano. Ilipofika wakati wa kujifungua, sikuwa na taarifa yoyote ama mafunzo yanayoweza kunifundisha ninavyoweza kujifungua"

"Nilikaa siku tatu hospitalini bila kujifungua nikiwa na uchungu; niliteseka na siku ya nne nesi mmoja alinifuata na kuniashiria kuwa nilale kitandani baadaye walikuja pembeni yangu manesi wengine  watatu walikuwa wanazungumza na sikujua nini walikuwa wanazungumza. Mmoja aliondoka akarudi kijana mdogo amenyoa panki tena alionekana kijana wa kisasa, nilipomuona nilijifunika na kujisitiri sehemu zangu za siri."

Anaendelea kusimulia: "Nikawa nawaona wanamwambia kuwa sisikii aje anisaidie yule kijana alikuja akiwa hana koti jeupe wala vipimo shingoni, ambavyo vinavyoonyesha kuwa anakuja kunisaidia. Ikanilazimu nijistiri na sikumpa ushirikiano, nilijifungua kwa tabu na baadaye mtoto alifariki dunia.

Serikali yaguswa

Kisa cha Subira kikamsukuma Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya aliyemwakilisha Waziri wa Afya, kusema kuwa jamii ya walemavu,  inakabiliwa na vikwazo na ubaguzi wanapotaka huduma zikiwamo za afya.

"Mmeona wenyewe namna wanavyojieleza na namna wanavyokumbana na changamoto za kukosekana kwa wakalimani wa lugha za alama. Ni vyema walemavu hawa wawe na wawakilishi wa kutosha kwa kufungua matawi katika mikoa yote ili kuwezesha wananchi kupata mikopo ikiwemo ile ya halmashauri ambayo ni asilimia 10 ya watu wenye ulemavu,"amesema.

Ameongeza:"Serikali imeendelea kuweka miundombinu wezeshi  kwa walemavu.  Wizara ya Afya itaendelea kuajiri wakalimani wa lugha za alama,  ni vema lakini pia hamasisheni watoto wenye ulemavu kujiunga na masomo katika vyuo mbalimbali,  ili kuondoa utegemezi.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz