Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkasa wa Ofisa Afya kupigwa mawe Dodoma

Mawe Jiwe.png Mkasa wa Ofisa Afya kupigwa mawe Dodoma

Wed, 15 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ofisa Afya wilayani hapa Mkoa wa Dodoma, Ismail Wabu anadaiwa kupigwa na wananchi kisha kutupwa katika pori lililopo Kijiji cha Igoyiwaji wilayani humo alipokuwa akitimiza majukumu yake ya kazi.

Awali, ofisa huyo na wenzake zaidi ya wanne, walikwenda Kijiji cha Igoyiwayi wilayani Mpwapwa kuendesha operesheni ya ujenzi wa vyoo bora na utunzaji wa mazingira.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema yuko kwenye kikao akitoka atampigia mwandishi wa habari hii.

Akizungumza kwa simu akiwa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, Wabu alisema tukio hilo lilitokea Novemba 9 mwaka huu.

Alisema awali, walikwenda kijijini humo saa 11 alfajiri na kumkuta kiongozi wa eneo hilo ambaye aliwaonyesha kaya zisizokuwa na vyoo.

“Yeye ndio (kiongozi wa kijiji) alikuwa anagonga milango ya watu na kuwahoji kama hawana vyoo kisha kuwaelekeza ofisini ili wakapate maelekezo ya utengenezaji wa vyoo,” alisema Wabu.

Alisema walipofika nyumba ya tatu kukagua hawakumkuta mtu, lakini wakaanza kurushiwa mawe huku miruzi ikisikika.

Wabu alisema lilijitokeza kundi la watu na kuzidi kuwashambulia kwa mawe na fimbo, hali iliyowafanya kukimbia, lakini alijikwaa na kuanguka chini na kushambuliwa zaidi.

“Nilisikia sauti ya kushinikiza auawe, auawe, nilipigwa kwa nguvu kichwani na kupoteza fahamu kisha kujikuta kwenye shamba nilipokuwa nimetupwa,” alisema Wabu.

Alisema alishtuka saa 12.00 asubuhi wakati wanawake wawili na mtoto walipokuwa wakipita katika eneo hilo kuelekea shambani.

Wabu alisema wanawake hao waliwaita watu, akiwamo mwenyekiti wa kijiji hicho waliofika kumchukua na kumpeleka hospitali.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Mwanahamisi Ally alisema sio mara ya kwanza kutokea kwa tukio kama hilo wilayani humo.

Alisema maofisa afya wengine waliwahi kushambuliwa na wananchi katika operesheni kama hizo miaka ya nyuma.

“Operesheni hiyo ni ya kawaida na inahusisha usafi tu na haikuanzia pale, ni mwendelezo na wala hawakutumia nguvu, walikuwa wanahamasisha tu. Kwa hiyo ni hali tu ya wananchi wasiotaka kubadilika,” alisema Mwanahamisi.

Alisema kila wakati operesheni kama hiyo inapoendeshwa baadhi ya wananchi hukimbilia msituni kukwepa kufikiwa na mkono wa sheria.

Mwanahamisi alisema kufuatia tukio hilo, watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya tuhuma za kuhusika na tukio hilo.

Septemba 2016, watafiti watatu kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Selian Arusha (Sari) aliuawa walipokwenda katika Kijiji cha Iringa Mvumi, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma kufanya utafiti wa udongo.

Watafiti hao waliuawa kwa kushambuliwa na silaha mbalimbali na kisha gari lao kuchomwa moto na wananchi wakiwatuhumu ni wanyonya damu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live